Menu
in , ,

Ancelotti afukuzwa Real Madrid

Real Madrid wamemfukuza kazi kocha wao, Carlo Ancelotti baada ya kushindwa kuwapatia taji lolote msimu huu.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez amethibitisha uamuzi huo na kusema kwamba kocha mwingine atateuliwa wiki ijayo.

Madrid wamevuliwa ubingwa wa Ulaya walioupata msimu uliopita, lakini hakuna klabu iliyopata kutetea ubingwa huo. Katika La Liga pia wamezidiwa nguvu na Barcelona ambao ndio mabingwa wapya.

Ancelotti mwenyewe alishakuwa na shaka iwapo angebaki Santiago Bernabeu baada ya mwenendo usioridhisha mwishoni mwa msimu kwa kikosi chake, na alitamka wazi hakuwa na uhakika na hatima yake.
Mechi yake ya mwisho, hata hivyo, ilimalizika vyema kwa kuwakandika Getafe 7-3 Mei 23.

Ancelotti ndiye aliwapa mafanikio Madrid msimu uliopita ambapo kwa mara ya 10 katika historia walitwaa ubingwa wa Ulaya – La Decima, Kombe la Fifa la Dunia kwa klabu na pia Kombe la Mfalme, maarufu kama Copa del Rey. Wapo waliodhani kwamba msimu huu waliteleza tu na kwamba angeachwa ili msimu ujao arekebishe mambo.

Hata hivyo, Perez amesema kwamba wameamua kuachana naye, lakini kwa kujiuliza swali na kujijibu:

“Ancelotti amekosea nini? Sijui. Lakini ukiwa Real Madrid unatakiwa kufanya mambo makubwa sana. Kazi ya ukocha Real Madrid ni ile ambayo unateseka sana muda wote. Nakumbuka mwaka wa tatu wa Jose Mourinho, alikuwa kocha aliyetumia muda wake mwingi zaidi kazini kwetu.

“Nasikia kwamba pamekuwa na makocha wengi Madrid, lakini hii hutokea pia kwa Atletico Madrid, Barcelona, Chelsea, Bayern Munich na Juventus.”

Magazeti ya Hispania yaliandika mwezi huu kwamba maofisa na wachezaji wengi wa Madrid walikuwa wanamuunga mkono Ancelotti, mmoja wa makocha wawili tu waliopata kutwaa makombe matatu ya Ulaya kila mmoja, mwingine akiwa ni Bob Paisley.

Cristiano Ronaldo, nyota wa Real na dunia, ni mmoja wa watu waliokuwa wakimuunga mkono Ancelotti kubaki, lakini Perez amesema licha ya hayo, hatamu kwa msimu wa 2015/16 zitashikwa na mtu mwingine.

Juzi tu Ancelotti alisema iwapo angebaki Bernabeu ingekuwa sawa, la angetulia bila timu kwa msimu mmoja, kama alivyofanya kocha wa sasa wa Bayern Munich, Pep Guardiola alipoamua kuondoka Barcelona.
Wapo waliokuwa wakidhani Ancelotti akiondoka angeweza kuingia Liverpool kuchukua nafasi ya Brendan Rodgers ambaye mwenyewe anasema amekalia kuti kavu.

West Ham United pia wanamtaka Ancelotti azibe nafasi ya Sam Allardyce anayeondoka baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
Rafa Benitez wa Napoli aliyepata kuwafundisha Liverpool kwa mafanikio makubwa anatajwa kama mtu anayeweza kuziba pengo la Ancelotti hapo Real.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version