Kuna kila dalili ya wingu jeusi kutanda kwenye ardhi ya Msimbazi. Ardhi ambayo imepambwa na udongo mwekundu na mweupe.
Ardhi ambayo inamiliki timu kubwa sana hapa nchini, timu ambayo ina mashabiki wengi sana nchini.
Na ndiyo timu hiyo hiyo kwa sasa inatuwakilisha Watanzania katika mashindano ya klabu bingwa barani Afrika.
Mashindano ambayo ni magumu sana, mashindano ambayo kunahitajika umoja mkubwa ndani ya timu.
Umoja ambao ungeunganisha hii pembe tatu Iwe imara, yani uongozi, mashabiki na timu kwa ujumla. Yani kuwe na muunganiko mkubwa hapa.
Kusiwe na kitu chochote cha kuitenganisha hii pembetatu. Pande zote tatu zishikamane. Lakini hili kwa sasa halionekani ndani ya Simba.
Simba kwa sasa hakuna maelewano, Manara atamrushia maneno shabiki, Shabiki naye atamrudishia maneno Manara na kuna wakati mwingine anamrushia maneno kocha.
Na kwa bahati mbaya kocha hana sehemu ya kusemea, anabaki kimya, hivo vita inabaki ya watu wawili tu, yani shabiki na Manara.
Hawa ni watu ambao wamekuwa na urafiki wa muda na uadui wa muda. Leo hii unawaona kama ni maadui lakini kesho utawakuta wameungana.
Kwanini nasema hivo ?, kuna wakati Haji Manara amekuwa akihamasisha sana mashabiki kwenda uwanjani na mashabiki hutii hamasa yake.
Kuna wakati Haji Manara hutumia muda mwingi sana kuwananga mashabiki wa Yanga na hapa ndipo urafiki wake na mashabiki wa Simba unakuwa.
Watafurahia pamoja, watamuunga mkono Haji Manara kuwanga hawa mashabiki wa Simba.
Lakini utengano huja pale timu inapokuwa inakosa matokeo chanya. Chanya inapokuwa inakosa matokeo chanya, ni watu wawili pekee ambao hushambuliwa.
Wa kwanza ni kocha, kwa sababu huyu siyo muongeaji sana hunyamaza kimya, na huwa anajua kabisa yeye ndiye anayewajibika na matokeo ya timu kwa sababu ni kocha.
Ukimya wake mara nyingi humuokoa huyu. Mashabiki wanapoona huyu kakaa kimya humgeukia Haji Manara , kimsingi huku ndiko huwa kuna vita kali sana.
Haji Manara ni mwanadamu ambaye amezaliwa kwa ajili ya kuongea. Hajazaliwa kwa ajili ya kukaa kimya, hajazaliwa kwa ajili ya kutojibu shambulio lolote kutoka kwa mtu yoyote.
Kimsingi hii vita kati ya mashabiki na Haji Manara inatokea wapi wakati Haji Manara siyo kocha au mchezaji ambaye anahusika moja kwa moja na matokeo ndani ya uwanja.
Jibu ni moja tu, Haji Manara amekuwa akiwaaminisha mashabiki vitu ambavyo kimsingi haviwezi kutekelezwa na timu ya Simba.
Alifikia mpaka hatua ya kuwaaminisha mashabiki kuwa timu ya Simba katika uwanja wa Taifa haiwezi kufungwa na Barcelona, Bayern Munich na Manchester City.
Hii ni kauli ya kutowapa heshima kila mpinzani wa Simba. Simba kuanzia kwa mashabiki mpaka timu imekuwa haitoi heshima yoyote kwa mpinzani wake yoyote.
Ndiyo maana waliadhibiwa baada ya kushindwa kuwapa heshima stahiki As Vita kule Congo. Hata kabla ya kwenda Congo walicheza na Azam Fc.
Hawakuwapa heshima stahiki Azam FC wakafungwa na Azam FC, na baada ya kutoka Congo walikuja kushiriki kwenye michuano ya Sportpesa.
Walitolewa na Bandari FC, sababu ni ileile tu kutowapa heshima wapinzani wao. Hata Mashujaa pia waliwatoa Simba kwenye kombe la TFF kwa sababu hawakuwapa heshima wapinzani.
Yani Simba imekuwa timu ambayo inajiamini sana, yaani inajiamini kupitiliza. Kuna wakati Wana Simba wanafikia hatua ya kuamini hakuna timu imara na bora duniani kote kama Simba.
Imani hii inaanzia wapi ?, simple tu , inaanzia kwa Haji Manara. Huyu ndiye anayewapiga upofu mashabiki wa Simba na siyo kocha wa Simba.
Kocha wa Simba hawezi kuwaaminisha mashabiki wa Simba kitu kisichowezekana hata siku moja. Ila kwa Haji Manara kwake yeye ni kawaida kuwaambia Simba ni zaidi ya Manch Manchester City.
Kwake yeye ni kawaida kusema pale ni Taifa ni machinjioni, yeyote yule anayekanyaga nyasi za Taifa ni haki yake kuchinjwa na Simba.
Hapa ndipo imani kubwa inapokuwa inawajaa mashabiki wa Simba, na masikini wa Mungu hatuna mashabiki ambao wanauwezo wa kuchambua baya na zuri wao humeza kitu moja kwa moja.
Tena hata bila kuchuja. Na Haji Manara anawajua vizuri, ashawasoma vizuri na yeye anawaendesha kama toyi. Anawapeleka kokote kule anapotaka.
Tatizo linakuja pale ambapo timu inapokosa matokeo chanya kwenye uwanja ambao awali ulisemekana ni uwanja wa machinjio.
Mashabiki huja mbele na hasira zao, ubaya zaidi hukosa sehemu sahihi za kurushia hasira zao. Ndiyo maana humshambulia mpaka kocha.
Mtu ambaye hausiki kabisa na ujinga huu, na kuna wakati mwingine humtaka kocha aondoke kwenye klabu yao na kumshau kabisa Manara ambaye ndiye anayewaaminisha wako Paris kumbe ni Tandale.