Mwishoni mwa wiki iliyopita mabingwa wa soka nchini Simba walikuwa jijini Kinshasa kumenyana na wawakilishi wa DR Congo katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi. Simba waliibuka na ushindi katika mchezo na kuwashangaza wengi kupata pointi tatu za kwanza ugenini na kuongoza kundi lao kwa muda.
AS VITA VS SIMBA
Hadi sasa kundi lao linaongozwa na mabingwa watetezi, A Ahly ya Misri wenye pointi tatu na mabao manne ya kufunga, wakati Simba wanashikilia nafasi ya pili wakiwa na pointi tatu na bao moja. AS Vita inafuatia kwa tofauti ya idadi ya kufungwa kwani El Marreikh ya Sudan ilichapswa mabao mengi na Al Ahly.
Katika mechi hiyo iliyopigwa katika dimba la Martyrs jijini Kinshasa kati ya AS Vita ya DR Congo na Simba ya Tanzania imenipa tafakari zaidi. Kwenye mchezo huo uliochezwa nchini DR Congo na kushuhudia Simba wakiibuka na ushindi dhidi ya wenyeji uliamsha shamrashamra kwa mashabiki wa Simba na wapenzi wa kandanda nchini.
Maelfu ya watu wamefuatilia mchezo huo kupitia televisheni iwe nchini Tanzania kote barani Afrika, lakini ni wachache wanaojadili ukweli mwingine kuhusu soka la Tanzania. Kwa sasa upo ukweli ambao unapanda ngazi taratibu na kuonesha mabadiliko ya kandanda nchini Tanzania.
Kilipotangazwa kikosi cha kwanza cha Simba katika mchezo huo upesi nilitazama orodha ya wanaoanza. Wachezaji saba wa kigeni walitajwa kwenye kikosi cha kwanza na kuvaa jezi za Simba zenye rangi nyekundu na nyeupe zenye neno kifuanui Visit Tanzania ikiwa ni mpango wa kutangaza sekta ya utalii nchini.
Wachezaji wa kigeni walikuwa Cletous Chama (Zambia), Larry Bwalya (Zambia),Pascal Wawa(Ivory Coast), Luis Miquissonne (Msumbiji), Tadeo Lwanga(Uganda), Chris Mugalu (DR Congo) na Joas Onyango (Kenya).
Kwenye kikosi cha kwanza wachezaji wazawa walikuwa wanne pekee; golikipa Aishi Manula, nahodha na beki wa kushoto Mohammed Hussein, beki wa kulia Shomari Kapombe na kiungo mkabaji Mzamiru Yassin.
Tukigeukia upande wa wachezaji wa akiba walikuwa Gadiel Michael (Tanzania), Kennedy Juma (Tanzania), Said Ndemla (Tanzania), Meddie Kagere (Rwanda), Bernard Morrison (Ghana), na Francis Kahata (Kenya).
Hiyo ina maana wachezaji wa kitanzania katika benchi la Simba walikuwa watatu pekee. Kati ya wachezaji hao wa akiba ni mtanzania Kennedy Juma, Mnyarwanda Meddie Kagere na Mkenya Francis Kahata ndiyo walipata nafasi ya kuingia dimbani.
Ukichukua wachezaji wanne wazawa walioanza na kumwongeza Kennedy Juma utagundua kuwa Simba ilimaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji watano wa Tanzania, kisha wachezaji wa kigeni walikuwa 9 waliocheza mchezo huo.
Yaani wachezaji saba walianza, kisha wawili Meddie Kagere na Kahata waliingia baadaye hivyo kujumuisha wachezaji wa kimataifa kufika 9 walioshiriki mchezo huo. Hii ina maana nafasi ya wachezaji wazawa ingeweza kupokonywa katika eneo lolote lile.
Katika kikosi cha Simba msimu huu 20202/2021 nafasi ambayo wazawa wana uhakika wa kudumu ni golikipa. Makipa wote wa Simba ni wachezaji wa Tanzania, Aishi Manula na Benno Kakolanya, nafasi zingine ni beki wa kulia na kushoto ambazo zina wanaoanza na kusaidiwa wote wazawa.
Hoja yangu ni kwamba, idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotamba katika kikosi cha Simba ni kubwa kuliko wachezaji wazawa. Kwenye mchezo dhidi yaAS Vita wachezaji wazawa walioshiriki mchezo ni watano, ikiwa na maana nafasi sita zilikuwa za wageni. Lakini wageni hao walishiriki ni wengi yaani 9 kuliko wazawa.
Katika mazingira ya kawaida wachezaji wa kigeni wanaopangwa basi wanakuwa na uwezo mkubwa wa kusakata kandanda. Pia suala la wachezaji wa kigeni kujazwa katika kikosi cha kwanza sio jambo la kushangaza.
Wakati Arsene Wenger akiinoa Arsenal iliitwa ‘Umoja wa Mataifa’ kwa vile alikusanya wachezaji karibu kila bara. Bara la Afrika, Asia, Ulaya, Amerika kusini,Australia yote yalikuwa na vipaji katika kikosi chake. Vile vile amewahi kupanga kikosi katika mchezo fulani bila kuwepo mchezaji mzawa yaani raia wa Uingereza.
Ninachotaka kusema ushindani baina ya wachezajiwa kigeni na wazawa ndilo jambo litakalotoa mchango na kuboresha uwezo wao. Wakati wachezaji wa kigeni watakuwa wanaimarisha timu zao za taifa, vilevile wazawa watakuwa wanachota ujuzi na kuhamishia kwenye timu ya Taifa kadiriwatakavyopata nafasi.
Ikiwa wachezaji wazawa wanataka kujifunza basi huu ni wakati ambao utaonesha wanavyowea kupambana katika soka. wachezaji wetu wanapokosa nafasi nje ya nchi huwa tunalalamika sana, lakini sasa wachezaji wa kigeni wameingia Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na maana sasa ushindani kamwe hawawezi kuukwepa kwa vile hata hapa utawafuata.
Wachezaji wa kigeni wanapokuja maana yake wanaimarisha viwango vya wazawa, ingawa kwa upande mwingine wanawanyima nafasi ya kupenya katika vikosi vya kwanza. Chukulia ujio wa Tadeo Lwanga wa Uganda, umesababisha Erasto Nyoni asugue benchi. Tunaweza kusema Nyoni umri unamtupa mkono lakini ni miongoni mwa wachezaji mahiri kila wanapopewa nafasi.
Kimsingi amsha masha ya wachezaji wa kigeni lazima itumike kuwazindua wazawa. Hakuna namna ambayo timu zitaacha kusajili wachezaji wageni na kupendelea wazawa kama hawana uwezo. TP Mazembe huwa inajaza wachezaji wengi wa kigeni, lakini mafanikio yake yanakuwa mali ya wananchi wa DR Congo.
Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa Simba mafanikio yake yanakuwa mali ya wananchi wa Tanzania. kwahiyo wachezaji wazawa wanatakiwa kuchukua tahadhari kama wanataka kung;ara katika soka mbele ya wachezaji wa kigeni maana wanatakiwa kuonesha ubora na viwango vya juu kuwazidi wageni hao.
Kinyume cha hapo ni vigumu. Naitazama amsha masha hiyo kama dalili ya kukumbushwa kuwa vipaji vya kigeni vitamiminika nchini kwakuwa vingi vinatafuta nafasi ya kupenya.