Wakati mjadala mkubwa unaendelea Ligi Kuu Tanzania kuhusu winga wa Yanga, Dennis Nkane kuchezeshwa kama beki wa kulia badala ya nafasi yake aliyopatia usajili, kumbukumbu kadhaa zimenijia. Mjadala huo unatokana na nafasi ya beki wa kulia katika mchezo wa kichapo cha mabao 3-1 alichopata bingwa mtetezi Yanga. Katika mjadala huo yapo mambo muhimu ya kiufundi yanapaswa kuoneshwa na hasa kurudisha kumbukumbu muhimu za uamuzi unaofanywa na makocha.
Likitajwa jina la Sir Alex Ferguson wengi wanalikumbuka raia huyo wa Scotland. Watasifia kila aina ya ujuzi aliokuwa nao mwalimu huyo wa kandanda. Ni mwalimu pekee aliyedumu kwa miaka 26 katika klabu ya Manchester United. Hakika alikuwa kiumbe cha aina yake na nguvu nzuri kuhimili mikiki ya kila msimu. Unapolitaja jina hilo haraka utarudi kwa wachezaji aliokuwa nayo. Kwenye vikosi vyake napenda kuyakumbuka majina mawili, Quinton Fortune raia wa Afrika kusini na Mikael Sylvester raia wa Ufaransa. Wakati nalikumbuka jina la Alex Furguson nitarudi nyumbani Tanzania na kuyakumbuka majina ya makocha wawili Marcio Maximo raia wa Brazil na Charles Boniface Mkwasa raia wa Tanzania. Kwa nyongeza ninamkumbuka Paolo Maldini yule mwamba wa AC Milan ya Italia. Sasa twendeni pamoja ili kuelewa kumbukumbu hizi.
Mikael Sylvester na Quinton Fortune
Alex Ferguson alikuwa akiwatumia wachezaji hao katika maeneo yao halisi. Lakini kadiri siku zilivyokwenda na mahitaji ya Manchester United wakati ule halikuwa jambo la ajabu kuwaona wakibadilishwa nafasi. Kwa asili Mikael Sylvester alikuwa beki mahiri wa kushoto na kipaji chake hicho ndicho kilimpeleka Man United toka kwao Ufaransa. Hata hivyo katika majukumu na uamuzi wa kocha Ferguson kuna wakati Mikael Sylvester akaishia kuchezeshwa beki wa kati.
Haikuwa mechi moja au mbili, bali mfululizo na nyakati zake za mwisho kabla ya kuondoka Man United alikuwa akipangwa nafasi ya beki wa kati. Uzoefu wake, maarifa yake na uwezo wake vilimpa nafasi ya kutumikia beki wa kati. Kwahiyo mabadiliko ya nafasi si mambo ya kushangaza. Kwa upande wake Quinton Fortune alikuwa mahiri kucheza kiungo wa kati. Uwezo wake mzuri wa kutumia mguu wa kushoto ulimfanya Alex Ferguson ambadilishe nafasi kutoka kiungo mkabaji hadi beki wa kushoto na wakati mwingine akapangwa winga wa kushoto. Katika hali hiyo hata alipokwenda timu ya Taifa ya Afrika kusini alipangwa nambari 10. Hawa ni wachezaji wenye namba zao za asili, yaani Fortune kiungo mkabaji, na Sylvester beki wa kushoto lakini wakapelekwa maeneo mengine kama anavyofanyiwa Dennis Mkane wa Yanga.
Paolo Maldini
Sifa yake kubwa ni bonge la beki wa kushoto. Italia inasifika kuwa na mabeki wakali zaidi barani Ulaya, kwahiyo Paolo Maldini naye alitokea nchi hiyo. Hata hivyo kadiri muda ulivyokuwa unaelekea mbele alipokuwa na umri wa juu ya 30 alikuwa akipangwa beki wa kati tofauti na nafasi yake aliyozoea ya kupambana na mawinga.
Fred Mbuna na Henry Joseph
Yanga wanampenda Charles Boniface Mkwasa kama staa wao wa zamani klabuni lakini pia kama kocha. Huyu ni kocha ambaye aliwahi kuchukua uamuzi mgumu wa kubadilisha Fred Mbuna kutoka ushambuliaji hadi beki wa kulia. Fred Mbuna alitumikia nafasi hizo Timu za Taifa na alipewa jukumu hilo kwa sabababu kocha Mkwasa aligundua maarifa aliyonayo. Fred Mbuna hakuwahi kulalamika lakini alikubali maagizo nja matakwa ya kocha.
Henry Joseph alisajiliwa Simba kutoka Mtibwa Sugar kwa sababu ya ubora wake wa kucheza namba sita. Lakini alipokuwa Taifa Stars chini ya Marcio Maximo alipangwa namba 7 yenye majukumu ya kuwa kiungo wa ulinzi katika mfumo wa 4-5-1. Henry Joseph alitumikia nafasi hizo na kuonesha namna mwalimu anaweza kugundua zaidi ya kipaji cha mchezaji. Kwamba utayari wake kutumikia eneo lingine linakuw ajambo la kawaida.
Aziz Andabwile na Gamondi
Yanga wamemsajili Aziz Andabwile kama kiungo mkabaji, lakini chini ya Miguel Gamondi nyota huyo anapangwa katika safu ya ulinzi. Kwamba ile nafasi iliyowapa sababu ya Yanga kumsajili imeongezewa majukumu kwa sababu mwalimu amegundua kitu cha ziada kwa nyota huyo. Kwa maana hiyo si Dennis Nkane pekee ambaye anabadilishiwa majukumu bali Aziz Andabwile ni miongoni mwa wachezaji wanaokubali kutimiza majukumu wanayokabidhiwa hata kama ni mapya.
Clement Mzize na Gamondi
Mshambuliaji Clement Mzize alisajiliwa Yanga kwa ajili ya kutupia mabao wavuni. Nafasi iliyowapa sababu Yanga kumsajili ilikuwa namba 9. Chini ya kocha Nasredine Nabi, Clement Mzie alipewa jukumu la kucheza kama mshambuliaji wa kati pekee ama wakati mwingine alikuwa kwenye mfumo wa kushirikiana na mshambuliaji pacha. Hata hivyo chini ya Miguel Gamondi tumeona Clement Mzize akipangwa hata winga wa kulia na ameonesha umahiri mkubwa.
Dennis Nkane na Lucas Vazquez
Kwa asili Dennis Nkane ni winga wa kulia ama kushoto. Hali kadhalika Lucas Vazquez ni winga wa kulia kwa asili. Nkane na Vazquez wamebadilishwa nafasi kutoka na sifa yao moja kuu; maarifa ama uwezo mkubwa wa kuwasoma wapinzani na kuwa na akili ya kushambulia. Hata hivyo linapofika suala la kujilinda au kufanya kazi kama beki halisi wa kulia wamepata changamoto. Mechi kadhaa Dennis Nkane amepangwa kama beki wa kulia badala ya nafasi iliyomtambulisha na kumpa ujiko Yanga, winga wa kulia.
Hata hivyo Dennis Nkane sio mchezaji mbaya ingawa sio beki mzuri wa kulia kama ilivyo kwa mwenzake wa Real Madrid Lucas Vazquez. Pale Real Madrid wametoka kuumizwa wiki hii katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwani wazee wenzao AC Milan walitumia udhaifu wa upande wa kulia wa Real Madrid kwa kumpanga Rafael Leao ambaye alimtetemsha nahodha msaidizi Lucas Vazquez na kumfanya awe mhanga wa kipigo cha mabao matatu. Miguel Gamondi anakitamani kipaji cha Dennis Nkane. Anatamani kuona winga huyo anatumia maarifa hayo kuanzia nafasi ya beki kuelekea eneo la adui.
Mechi alizopangwa mara nyingi Nkane alikuwa akivuka mstari wa eneo la katikati ya dimba pembeni hucheza kama winga kwani kasi,chenga na maarifa huwafanya wapinzani warudi nyuma. Hali hiyo iko kwa Lucas Vazquez pia akivuka mstari huo anakuwa mchezaji hatari. Ni kama mawinga wa ziada kwenye mashambulizi sababu ni asili yao kushambulia (Offensive).
Hasara ya wachezaji kama Dennis Nkane na Lucas Vaszquez ni pale timu inaposhambuliwa; sio wachezaji wepesi wa kucheza kwa umahiri kama walinzi (Defensive). Mfano Lucas Vazquez alikuwa mahiri kama beki wa kulia enzi za Zinedine Zidane akiwa kocha, lakini wa sasa anacheza zaidi kutegemea timu inaendeshwaje. Wapinzani wanayelenga maeneo dhaifu kwahiyo hilo nalo liliwapa mwanya Tabora United kufanya vitu vyao. Yacouba Sogne anao uzoefu na aliona namna eneo hilo linavyo mwanya.
Bernado Silva kwa Pep Guardiola
Mpira wa miguu unachota maarifa. Kwahiyo wapo wachezaji wanaiga kutoka kwingine pamoja na makocha wao nao wanaweza kuiga mbinu kutoka kwingine. Sababu za kuwatumia wachezaji kwenye nafasi zisizo za asili yao ni kutambua vipaji na maarifa yao. Pep Guardiola alifanya jaribio gumu la kumpa Bernado Silva kucheza eneo la kiungo mkabaji dhidi ya Chelsea kwenye fainali ya Ligi ya Mbaingwa misimu kadhaa iliyopita. Chelsea walipokuwa chini ya Thomas Tuchel walifanikiwa kumnyamazisha Pep Guardiola, huku maelfu wakimlaumu kushindwa kuanza kikosi cha kwanza na kiungo halisi mkabaji. Pengine mkakati wa kocha ulikuwa mzuri, lakini haukuleta matunda yaliyotakiwa kwa mchezo husika.
Hitimisho
Hali kadhalika uamuzi wa Miguel Gamond kumpa beki wa kulia Dennis Nkane ni kuthamini kipaji chake kwa namna nyingine. Badala ya kumsugulisha benchi mwalimu amegundua anaweza kumtumia kama silaha yake kwenye mapambano ya nchi mbalimbali. Lakini vilevile ni kujaribu kumpa nafasi kwenye kikosi chenye ushindani kwa kutumikia majukumu mengine, muhimu ni mbinu anazotaka mwalimu dhidi ya wapinzani anaokutana nao.