Mashabiki wa soka wanamuona Louis van Gaal kama shujaa wa soka katika fainali za kombe la dunia mwaka huu nchini Brazil.
Lakini Van Gaal hajafanya kitu kipya. Na makala haya yatakueleza sababu.
Golikipa Tim Krul ameandika rekodi yake kuwa golikipa wa kwanza katika fainali za Kombe la Dunia kuwa na kazi ya kuokoa penalti pekee.
Kipa huyo wa Newcastle United ya England akiwa benchi dakika chache kabla ya hatua ya kupigiana matuta na Costa Rica, kocha Louis van Gaal aliamua kufanya mabadiliko kwa kumtoa golikipa namba moja Jasper Cillessen.
Lazima tuwapongeze Uholanzi kwa kufanya kazi nzuri, lakini wamekutana na changamoto nzuri tuliyotarajia katika soka.
Mpira wa miguu sasa unazidi kuchanua kwa mataifa madogo, nadhani hata Taifa Stars sasa inaweza kufanya kitu kwenye mashindano yake.
Hata hivyo, mabadiliko ya golikipa wa penalti yaliyofanywa na kocha wa Uholanzi Louis van Gaal kwangu mimi wala hayakunishtua.
Ni jambo ambalo tumezoea kuliona katika soka barani Afrika kuanzia mwaka 2005. Ligi ya Mabingwa Afrika imekuwa na msisimko wake pamoja na kuweka rekodi ya kipekee.
Katika klabu ya Enyimba ya Nigeria kuna makipa wazuri wamewahi kuichezea. Miongoni mwa makipa hao alikuwa Chijioke Ejiogu.
Ejiogu alionesha umahiri wake mwaka 2010 wakati akiwa ndani ya jezi za Enyimba, lakini hakuwa kipa maalumu wa kuokoa penalti.
Nakumbuka katika michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF) mwaka 2010 Chijioke Ejiogu aliibuka shujaa wa Enyimba katika mchezo wao dhidi ya AS Vita ya DRC na kufuzu hatua raundi ya pili.
Lakini pambano gumu zaidi kwa kipa huyo lilikuwa dhidi ya Peoples Elephant pia ya DRC. Kipa huyo aliokoa penalti tatu kati ya tano katika pambano hilo.
Umahiri wa Ejiogu hakuwa na maana yeye ni golikipa wa penalti. Tunapomzungumzia golikipa wa penalti tuna maana anakuwa na kazi maalumu ya kuokoa penalti tu.
Kipa huyu huingizwa dakika chache kabla ya pambano kumalizika huku likiwa na mwelekeo wa kufikia hatua ya matuta.
Tim Krul aliingizwa uwanjani ikiwa imesaliwa na dakika moja na nusu kumalizika kwa pambano kati ya Uholanzi na Costa Rica.
Kocha Louis van Gaal anaweza kusifiwa, lakini wapo wengine ambao waliifanya kazi yao kwa ufasaha kabla yake tena kwa miaka ya karibuni tu.
Enyimba ikiwa chini ya kocha mzawa Alphonsus Dike aliyedumu kuanzia mwaka 2005 hadi 2006 ilikuwa na kipa wa penalti.
Ingawa nafasi yake ilichukuliwa na kocha Maurice Cooreman kuanzia oktoba mwaka 2006 bado Enyimba ilikuwa na utamaduni wake ulioeleweka kutokana na kuwa na kipa wa penalti.
Kwahiyo Enyimba ni klabu ya kwanza kumtumia golikipa wa penalti. Katika michuano yao ya Ligi ya Mabingwa walikuwa na tabia hiyo kama aliyofanya Louis van Gaal kumwingiza Tim Krul.
Mara nyingi Vincent Enyeama alikuwa anatolewa dakika chache kabla ya hatua ya matuta na nafasi yake kuchukuliwa na Dele Aiyenugba.
Nadhani mashabiki wa soka watakumbuka mechi ya nusu fainali ya Ligi ya mabingwa kati ya Enyimba na Etoile du Sahel ya Tunisia.
Pambano hilo lilifikia hatua ya matuta baada ya matokeo ya jumla ya emchi zote mbili kwenda sare 3-3.
Zilipokaribia dakika za kupigiana penalti, Enyimba walimtoa golikipa wao Vincent Enyeama na nafasi yake kuchukuliwa na golikipa wa penalti Dele Aiyenugba.
Katika mchezo huo Dele Aiyenugba aliweza kupangua penalti ya Ben Frej na kuipa ushindi Enyimba wa penalti 5-3.
Pengine jambo hilo tunaweza kusema walibahatisha, lakini benchi la ufundi la Enyimba lilikuwa makini na uteuzi wa kipa wa penalti.
Katika mchezo mwingine wa nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika, Enyimba walirudia jambo hilo walipocheza dhidi ya Esperance ya Tunisia pia.
Muda ulipoyoyoma benchi la ufundi likamwinua kipa wao wa penalti Dele Aiyenugba ambaye aliokoa penalti mbili na nyingine mbili zikaota mbawa.
Umashuhuri wa Dele Aiyenugba haukuwa katika kudaka ndani ya dakika 90, bali aliyekuwa anafanya kazi hiyo ni Vincent Enyeama.
Ulimwengu wa soka unatufundisha hayo na makocha wanaweza kuchukua mbinu za wenzao. Louis van Gaal kama kocha lazima atakuwa anaifahamu Enyimba na ufundi wao.
.