Baada ya siku kadhaa kuthibitishwa kwa habari za Kampuni ya matairi ya Binslum kuingia mkataba wa kuidhamini klabu ya Mbeya City, wafanyabiashara kutoka makampuni mbalimbali wameendelea kumiminika kuidhamini klabu hiyo ya jijini Mbeya.
Binslum Tyres Co.Ltd imeingia mkataba wa miaka miwili wenye kiasi cha pesa kisichopungua milioni 360 ambapo, klabu hiyo itapewa kiasi cha milioni 180 mwaka wa kwanza na kiasi kilichobakia, kitamaliziwa mwaka wa pili wa mkataba huo.
Timu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya jiji la Mbeya, inaonekana kuwashawishi wadhamini wengi kutokana na ubora wao uwanjani na uongozi wenye kutambua majukumu yake.
Mbeya City licha ya kuwa wageni kwenye ligi kuu, walifanikiwa kumaliza kwenye nafasi ya tatu huku timu ambazo walipanda nazo daraja za Rinho Rangers ya mkoani Tabora na Ashanti United kutoka Dar es salaam zikiambulia kushuka daraja.
Akizungumza kwa nyakati tofauti, katibu wa Mbeya City, bwana Emmanuel Kimbe, amesema kuna wadhamini lukuki ambao wamejitokeza kutaka kuingia mikataba na timu hiyo ili kuweza kutangaza biashara zao. Mbeya City wamefanikiwa kujipatia umaarufu hapa nchini baada ya kufanya vizuri msimu uliopita huku wakipata sapoti ya nguvu kwenye kila kiwanja wachokwenda kucheza mechi.
Timu hiyo inayopatikana mitaa ya Soweto na Mwanjelwa jijini Mbeya, hivi karibuni imetoka kushiriki michuano mipya ya CECAFA maarufu kama Nile Basing na kutinga hadi kwenye hatua ya robo fainali kabla ya kung’olewa na timu ya Victoria kutoka nchini Uganda.
Mbeya City inaonekana kuwa kwenye mwelekeo mzuri na hapo baadae kuja kutoa wachezaji wengi kwenye timu ya taifa kutokana na msingi wa timu hiyo kujengwa kwenye kuwatumia zaidi wachezaji wanaotoka ndani ya nchi ambapo mpaka sasa, Taifa Stars inamjumuisha mchezaji mmoja tu wa timu hiyo, mshambuliaji Mwagane Yeya.