Menu
in ,

AJIB NI MCHEZAJI WA MECHI NDOGO

Tanzania Sports

Msimu jana Real Madrid ilibeba ubingwa wake wa tatu mfululizo wa ligi ya mabingwa ulaya. Ubingwa ambao aliubeba kwa kutumia nguvu kubwa sana kwa sababu ya aina ya timu ngumu alizokutana nazo kabla hajaenda kukutana na Liverpool katika hatua ya fainali.

Inawezekana kabisa Liverpool hakuwa amepata vipimo vingi vizuri kama ambavyo Real madrid alivyopata kabla ya kuingia fainali. Alikutana na vigogo haswa!, vigogo vya ulaya ambavyo ni mabingwa wa nchi zao lakini alifanikiwa kuvitoa, hii ndiyo maana ikaitwa ligi ya mabingwa unakutana na mabingwa ili ushinde mbele ya mabingwa na uchukue kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya.

Lakini huwezi kufanya vyote hivi bila kuwa na wachezaji ambao ni mabingwa, wachezaji ambao huibeba timu yako hata nyakati ngumu ambazo unaona kabisa jahazi linahitaji usaidizi maalumu!, ndiyo maana Gareth Bale aliibeba Real Madrid katika hatua ya fainali, lakini kabla Cristiano Ronaldo aliibeba kwenye mechi dhidi ya Juventus na Bayern Munich (hawa ni mabingwa wa Italy na Ujerumani).

Lakini kabla ya kukutana na hawa, Real Madrid alikutana na PSG, mabingwa wa Ufaransa. Timu ambayo imesheheni mastaa wengi ambao wanalipwa pesa ndefu sana kutoka kwa matajiri wa visima vya mafuta katika falme za kiarabu. Pesa ambazo ziliwakutanisha Mbappe , Cavan na Neymar kwa pamoja.

Neymar ambaye wengi tulimtabiri kwa kiasi kikubwa kuwa ndiye mtu sahihi ambaye atakuja kuvunja utawala wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Utawala ambao ulidumu kwa muda wa miaka 10 kabla ya Luka Modric kuuvunja mwaka.

Waliweka utawala wao kwa sababu waliamua kuwa wakubwa, walicheza na kujituma ipasavyo kwenye kila mechi ambayo miguu yao ilikanyaga nyasi za viwanja mbalimbali. Kwao wao (Cristiano Ronaldo na Lionel Messi) hawakuwa na mechi kubwa au ndogo ndani ya miaka kumi ya utawala wao.

Walizibeba timu zao kwenye kila aina ya mechi, na kwenye mechi kubwa walionesha ufalme wao haswaa!, kipindi ambapo timu imebanwa na inahitaji ushindi kwa namna yoyote wao ndiyo walikuwa wanaibuka kuwa mashujaa, walitengeneza furaha kwa mashabiki wao kwa kufunga magoli ambayo ni muhimu sana kwenye timu kwenye mechi ambazo ni ngumu na kubwa.

Hii ni shule tosha, ni shule ambayo wachezaji ambao wanatamani kuwa nyota wanatakiwa kukaa chini na kujifunza namna ya kuzibeba timu zao kipindi ambacho timu zinahitaji msaada wao. Shule hii Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wameitoa sana kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Na kizuri zaidi, kwenye mechi ya ligi ya mabingwa barani ulaya msimu uliopita kati ya Real Madrid na PSG, Cristiano Ronaldo alitumia muda wake kumsogezea darasa huru Neymar. Alimletea kila aina ya vitabu ili ajifunze jinsi ya kuibeba timu nyakati ngumu.

Mechi ile PSG ilimwihitaji sana Neymar, ilihitaji ukomavu wa miguu ya Neymar ili kuivusha na kwenda hatua inayofuata, lakini cha kusikitisha zaidi ilikuwa ngumu kwa Neymar kufanya vile . Hakuelewa chochote kile alipokuwa anaambiwa kwa vitendo na Cristiano Ronaldo kuwa anatakiwa kukomaa zaidi na kuibeba timu katika mechi kama hizi kama kweli anatamani kufika sehemu ambayo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo walipo.

Hakuelewa kabisa!, aliamini katika ubinafsi kila alipokuwa anapata mpira, alikuwa anatumia muda mrefu sana kukaa na mpira bila faida yoyote kitu ambacho kilikuwa kinaharibu kwa kiasi kikubwa mijongeo ya mashambulizi ya timu ya PSG.

Tulijua angejifunza zaidi katika mechi hiyo, hata pale tuliposikia kuwa ataenda Russia na timu ya taifa ya Brazil tuliamini kuwa ni wakati sahihi kwake yeye kuonesha kwa vitendo mafunzo ambayo aliyapata kwenye mechi ile dhidi ya Realmadrid, lakini ilikuwa tofauti na matagemeo yetu kabisa!, alicheza katika kiwango cha chini!, akashindwa kuibeba timu ikawa ni mtu ambaye alikuwa akianguka kila alipoguswa.

Uzito wa timu ulimwelemea kwa sababu ya yeye kutotaka kuwa mkomavu katika maamuzi yake ndani ya uwanja. Mara nyingi tunajua binadamu hujifunza kutokana na makosa, hivo tulizidi kuamini Neymar atajifunza sana kutokana na kile kilichotokea kwenye kombe la dunia. Tukaamini ataamua kuwa mtu mzima na kusimama imara kwenye vita kubwa dhidi ya mataifa makubwa.

Mechi dhidi ya Liverpool ilikuwa kipimo chake cha kwanza, hakuonesha ubaba wa familia kwenye mechi hiyo. PSG imwihitaji sana ila yeye alikuwa akiikimbia kwa sababu ya kujifanya kijana wakati alikuwa amepewa majukumu ya ubaba wa familia.

Kitu hiki pia kipo kwa Ibrahim Ajib “Migomba”. Inawezekana huyu akawa na kipaji kikubwa sana, kipaji ambacho kimemfanya kujizolea mashabiki wengi sana hapa nchini lakini anakosa kitu kimoja tu ambacho kina mfanano mkubwa sana na kitu ambacho anakosa Neymar.

Huwezi kubwa mkubwa kama hujaweza kupambana na wakubwa wenzako!, huwezi kujisifu mbio kwa kuwashinda viwete. Unatakiwa upambane na wakimbiaje ambao wanamiguu imara kama yako hapo ndipo ukubwa wako utakapoonekana. Hapa ndipo Ajib anapoanza kukosa sifa za kuwa mkubwa.

Mechi nyingi kubwa hupotea sana, ni ngumu kuibeba timu yake kipindi ambacho inacheza na timu kubwa. Upiganaji hupungua!, ubunifu hufifia kwa kiasi kikubwa na uwezo wa kufunga hutoweka kabisa na kubaki kuwa na Ajib wa kawaida sana, Ajib ambaye hafananii na Ajib wa mechi dhidi ya Lipuli, Stand United, Mbao Fc n.k

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version