Nani anaweza kuwa nahodha Man United?
KOCHA wa Manchester United, Eric Ten Hag amemwambia Harry Manguire hatakuwa nahodha wake msimu ujao. Kwahiyo cheo hicho amepokonywa. Hii ina maana hata sasa Manchester United nayo inaelekea kwenye utamaduni wa mbovu wa majirani zao Manchester City ambao unahodha hauna mwenyewe na sifa za kukabidhiwa kitambaa hicho ni kama zimesiginwa.
Kila mara nahodha wa Manchester City huwa anakuwa kwenye msimu wa mwisho kuondoka, ilikuwa hivyo kwa mwamba Vincent Kompany akarudi kwao Ubelgiji, ikaja kwa Fernandinho akafungasha viarago kwenda Brazil, na msimu umekwisha sasa tumeona kwa Ilkay Gundogan naye ameondoka zake kwenda Barcelona. Inaelekea nahodha ni Pep, kocha ni Guardiola tu. Maajabu!
Sasa kwa majirani zao Manchester United nao ni kama wameanza kuachana na utamaduni wa heshima ya nahodha. Kuondolewa Harry Manguire inaweza kuchambuliwa kuwa hana uhakika wa namba kikosi cha kwanza. Lakini Harry Manguire huyo amekuwa mwamba katika mfumo wa kikosi cha timu ya Taifa ya England maarufu kama Three Lions chini ya kocha Gareth Southgate.
Kunyang’anywa unahodha ni kitu kinachohuzunisha lakini kipi kinafaa kwa kikosi cha Manchester United kwa sasa? Ni kweli lazima wawe na nahodha mwenye sauti uwanjani. Lazima wawe na nahodha ambaye anapigania namba yake. Lazima wawe na nahodha ambaye ni halisi, uwanjani yupo na kiwango awe nacho. Lakini Manguire amekuwa beki wa ‘tia maji’, leo atacheza vizuri, kesho anaharibu na makosa kibao.
Kwa maana hiyo Harry Manguire japo amehuzunika kuporwa unahodha lakini kocha wake amekuwa muungwana. La ajabu ni kwamba Harry Manguire bado anataka kupambania namna yake kikosini mbele ya Raphael Varane na Lisandro Martinez.
Nani anaweza kuwa nahodha Man United?
Bruno Fernandez
Hana haiba hata robo ya Roy Keane, lakini ni mchezaji ambaye amewaongoza vizuri wenzake msimu uliopita. Kitambaa cha unahodha kilikuwa kwake muda mwingi na haitshangaza akiteuliwa rasmi kuwa nahodha wa timu hiyo. Bruno hamwachi mwamuzi bila kumpigia kelele pale anapoona wanaonewa. Ni nahodha anayezungumza na kufoka uwanjani.
Anajitahidi kuhamasisha na anaweza kupangwa nafasi yoyote ya kiungo; upande wa kulia au kushoto, nyuma ya mshambuliaji au kiungo nambari nane. Tatizo lake ni moja tu; kufoka kupitiliza hali inayomfanya abwatukiane na waamuzi hivyo kulimwa kadi za njano. Anajua pa kuanzia kufoka ila sio pa kumaliza.
Carlos Casemiro
Mwamba kutoka Brazil. Kwa msimu wake wa kwanza unamwona kabisa ana sifa nyingi na mkubwa kwa wasifu kuliko wachezaji wote waliopo katika kikosi cha Manchester United. Casemiro ana uzoefu mkubwa kiwanjani. Vitendo vyake huhamasisha, anaamrisha timu inapozuia na kuzungumza na waamuzi kwa staha. Huwezi kumkuta akimfokea mwamuzi au kubwatuka tu. Ni msiri pia kwani huficha mdomo wake kila anapozungumza na mwamuzi ili ibakie siri yao.
Ni mchezaji ambaye anaongoza kikosi kama injini inayoimarisha timu na kuipa uwiano wa kushambulia na kujilinda. Lakini ana kosa sifa moja muhimu; hana muda mrefu katika kikosi cha Manchester United. Ana msimu mmoja tu tangu ajiunge na timu hiyo. Lingine ni nafasi yake, uchezaji wa kiungo mkabaji wenye uhuni mara kadhaa (Dark arts) umemzawadia kadi nyekundu. Hivyo timu kucheza bila nahodha wake mwenye ushawishi ni tatizo.
Marcus Rashford
Ni kijana mkimya kiwanjani. Ukimya wake huenda ukamnyima nafasi ya kuwa nahodha wa timu. Ni mchezaji mwenye sifa zote muhimu ikiwemo kuichezea timu hiyo muda mrefu kuliko Bruno na Casemiro. Huyu ni zao la Manchester United ambalo wanaweza kujivunia hata pale atakapotangazwa kuwa nahodha mpya wa timu.
Luke Shaw
Ni beki wa kushoto ambaye ni kivutio kikubwa kwa uchezaji wake. Ni mchezaji ambaye amedumu muda mrefu Manchester United. Kwa haiba si mchezaji mkorofi au mzungumzaji kiwanjani, labda kutokana na kutokuwa na madaraka ndani ya dimba. Lakini Shaw ni miongoni mwa wachezaji wenye mvuto na wanaweza kuteuliwa kuwa nahodha wa msaidizi wa pili au wa tatu hivi.