*Ghana, Burkina Faso, Ivory Coast safi
*Zambia kuwakamata nyota waliotoroka
Wakati hakuna nchi ya Afrika iliyojihakikishia kucheza Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil, Ghana wamepiga hatua kubwa na muhimu.
Black Stars waliwafyatua Misri mabao 6-1 nyumbani na kujijengea mazingira mazuri ya kufuzu watakaporudiana mwezi ujao.
Wanaweza kufaidi zaidi iwapo Fifa wataamua mechi ichezwe nje ya Misri kutokana na machafuko ya kisiasa kama ambavyo Ghama wameomba.
Nchi 10 zinacheza mechi mbili kuchuja kupata tano zitakazokwenda Brazil, ambapo katika mechi za awali Algeria walifungwa mabao 3-2 na Burkina Faso, Ivory Coast wakawafunga Senegal 3-1, Ethiopia wakafungwa 2-1 nyumbani kwao walipokabiliana na Nigeria, huku Tunisia na Cameroon wakiambulia suluhu.
ZAMBIA YAAGIZA WACHEZAJI KUKAMATWA
Nyota watatu wa timu ya taifa ya Zambia wameingia matatani baada ya kukacha mechi dhidi ya Brazil kwa madai ya ugonjwa.
Wachezaji hao wanaochezea TP Mazembe walidanganya kisha wakatoroka kwa kuvuka mpaka kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kuchezea klabu yao hiyo.
Kutokana na kitendo hicho cha utovu wa nidhamu, ambapo Brazil waliwafunga Zambia 2-0 kwenye mechi ya kirafiki iliyofanyika China, Zambia imeamuru kukamatwa kwa wachezaji hao na kurejeshwa nyumbani kukabiliana na mkono wa sheria.
Wachezaji hao ni Rainford Kalaba, Stoppila Sunzu na Nathan Sinkala ambao klabu yao ya TP Mazembe imekuwa ikisisitiza kwamba ni majeruhi na kusababisha mvutano na Serikali ya Zambia.
Wachezaji hao walifanyiwa uchunguzi wa kiafya jijini Lusaka, kisha FA ikaamua kwamba walikuwa fiti hivyo wasafiri kwenda Beijing na wenzao lakini TP Mazembe walizidi kudai wachezaji wao warudishwe Kongo.
Serikali ya Zambia iliingilia kati kwa kuwapokonya pasi zao za kusafiria ili wasiweze kusafiri, kwenda Lubumbashi yalipo makao makuu ya klabu yao.
Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha wachezaji hao watatu walifanikiwa kuvuka mpaka wa nchi mbili hizo na wanaaminiwa kwamba tayari wapo nchini Kongo wakiitumikia klabu yao na kupoteza uzalendo kwa taifa.
FA ya Zambia imeiandikia Fifa ikilalamikia kitendo cha Mazembe licha ya kuwa kwenye tarehe za mechi za kimataifa wakati serikali ikiagiza wakamatwe.
Zambia ndio walikuwa mabingwa wa Afrika mwaka jana na mechi dhidi ya Brazil ilikuwa ya kwanza chini ya kocha wa muda, Patrice Beaumelle aliyechukua nafasi ya Herve Renard siku chache zilizopita.
Zambia walishatolewa katika hatua za kufuzu Kombe la Dunia na pia hawakufanya vyema kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika.