Menu
in

Afrika itakavyosuka au kunyoa Olimpiki 2012, London.

*Nini matarajio ya Watanzania?
*Pata takwimu za maandalizi ya kila nchi

MICHEZO ya Majira ya Joto ya Olimpiki ni fursa muhimu kwa wadau wa michezo kuonyesha umahiri wa nchi zao katika medani mbalimbali.
Afrika, moja ya mabara yenye vipaji vingi kwa asili, imejiandaa kwa namna tofauti, kutegemea mwamko wa nchi moja hadi nyingine.

Zipo ambazo zimekuwa na sifa kubwa ya ushiriki, lakini zinazojivunia rekodi ya ushindi wa medali kedekede ila si nyingi sana.
Safari hii michuano inafanyika Uingereza, moja ya nchi kubwa na mshirika mkubwa wa Afrika, vumbi likitimka kuanzia Julai 27 hadi Agosti 12 jijini London, mara ya tatu kwa jiji hili kuiandaa.

Wakati miezi ikikatika kuelekea sherehe za ufunguzi na hatimaye wanamichezo kuonyesha umahiri wao, Waafrika hawajabaki nyuma katika kujiandaa, hata kama ni kwa uchache.

Kwa bahati mbaya, ni katika mwonekano hasi nchi kama Tanzania inaonekana, kwa sababu ya maandalizi mabovu, yanayosababisha kuwakilishwa na wanamichezo wachache, lakini pia ndoto ya kuzoa medali kufifia hata kabla mashindano kuanza.
Kila miaka minne watu wamekuwa wakisubiri kwa hamu mtu wa kuvunja rekodi za akina Filbert Bayi na Suleiman Nyambui.

Wawili hawa ndio sura ya Tanzania, linapokuja suala chanya la Olimpiki, kwani ndio pekee walioipatia nchi medali, tena za fedha na wote katika riadha kwenye michuano ya mwaka 1980.
Bayi alipata medali yake kutokana na ushindi wake katika mbio za mita 3,000 kwa wanaume kuruka viunzi wakati Nyambui alishinda katika mbio za wanaume mita 5,000 – wote kwenye mashindano yaliyofanyika Moscow, Urusi.

Miaka zaidi ya 30 leo, bado hakuna Mtanzania aliyeweza kufikia, achilia mbali kuvunja rekodi hizo, au wale wa michezo mingine kung’aa.
Simulizi za maandalizi mabovu ziliendelea kama ilivyotarajiwa katika kupata washiriki wa michuano ya mwaka huu.

Hata baadhi ya wanamichezo walipotangaza au kutangazwa kwamba wangeshiriki mashindano haya, palibakia utata, huku mamlaka husika ndani ya nchi ikiwa haina uhakika na kufuzu huko.

Hilo liliwapata wanariadha Mseduki Mohamed nan Faustine Mussa, ambao ilibidi wabaki wamepigwa butwaa hadi pale Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) lilipokuja kutoa tamko.

IAAF ilithibitisha kwamba wawili hao walishiriki kwenye mashindano wanayo yasimamia, na kwamba walifanya vizuri na kufuzu kushiriki kwenye michuano hii ya Olimpiki.
Mseduki alishiriki kwenye michuano iliyofanyika nchini Poland Mach 29 wakati Faustine alicheza Ujerumani Mei 6 na kufanikiwa kufikia viwango.

Ilivyotokea ni kwamba, baada ya wanariadha hao kusema walishiriki mashindano na kufuzu kwa ajili ya ichuano hii kupitia Chama cha Riadha Tanzania (AT), Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) haikuweza kuidhinisha madai hayo, kwa sababu haikuwa na uthibitisho, hadi IAAF walipowaandikia rasmi.

Kwa hali ilivyo, Tanzania itawakilishwa na wachezaji sita kwenye Michuano ya Olimpiki. Wanariadha watakuwa wanne. Watakaoungana na hao wawili wa mwanzo ni Zakia Mrisho na Samson Ramadhan walio kambini tayari.

Michezo mingine ni ngumi, ambapo bondia mmoja, Seleman Kindunda ataiwakilisha nchi kama itakavyokuwa kwa Magdalena Moshi kwa upande wa kuogelea. Huyu amekuwa kambini nchini Austria anakosomea masuala ya utabibu michezoni.

Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi (aliyenyakua media ya fedha mwaka 1980), anasema kwamba Tanzania itakuwa na msafara wa watu 13 kwenye mashindano hayo.
Hao wanatarajiwa kuondoka nchini kwa safari ya London kati ya Julai 6 na 7 na kuweka kambi katika Chuo cha Bradford kilichopo Leeds.

Katika msafara huo, watakuwapo makocha wawili – mmoja wa kuogelea na mwingine wa ngumi na wengine watakaoambatana na timu ni viongozi.
Ikiwa maombi ya Chama cha Kuogelea Tanzania yatakubalia na Kamati ya Kimataifa ya Olimpki (IOC), Tanzania itapata uwakilishi zaidi, ambapo mwogeleaji mmoja wa kiume ataongezwa.

Hiyo ndiyo Tanzania, maandalizi na picha inayotolewa kwa ajili ya matokeo kwenye michezo hii muhimu, ambayo nchi zinawekeza vilivyo, kwani ni jukwaa muhimu la kujitangaza na kujipatia sifa.

Na katika Bara la Afrika pia, maandalizi ya wanamichezo kwa ajili ya Olimpiki si haba, ndiyo maana katika nchi mbalimbali unaweza kukuta mashindano ambayo hukujua kama yapo – kumbe ndiyo ya mchujo kwa ajili ya Olimpiki.

Vyombo vya habari katika nchi husika pia, vimejikita kwa sasa kufuatilia na kutoa habari za wanariadha wake zaidi, wakijua ni mbegu zinazopandwa sasa zitakazovunwa Julai na Agosti jijini London.

Ethiopia na Kenya ndizo nchi za Afrika zinazopewa nafasi kubwa zaidi za kufanya vizuri kwa kuzoa medali kwenye Olimpiki mwaka huu.
Wanamichezo wake si wa kawaida na programu zao za Olimpiki hupewa uzito mkubwa, mazoezi yakiwa ya kina, ili kuhakikisha nchi zao haziaibiki na hazipendi kushiriki tu bali kushindana na kujipa nafasi kubwa ya kushinda.

Kuna nchi kama Togo ambazo zipo chini, zikituma wanamichezo wawili wawili tu, kwa sababu haziwezi kumudu kupeleka wengi zaidi hata kama wangekuwa wamefuzu.
Ngumi ni moja ya mashindano yanayowezesha nchi za Afrika zisizokuwa na umaarufu michezoni kuwakilishwa kwenye Olimpiki.

Hapa zinazungumziwa nchi kama Algeria, Botswana, Cameroon, Swaziland na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ukiacha ngumi, kuna michezo mingine kama badminton, taekwondo na judo ambayo hutokea kuibua watu wasiotarajiwa kutoka maeneo yasiyotarajiwa pia na kutinga kwenye Olimpiki kama utani.

Wanamichezo kutoka Sudan Kusini na Somalia, kwa mfano, watashiriki Olimpiki, licha ya maandalizi duni nyumbani na ukosefu wa udhamini kwao.
Angola ndiyo nchi yenye timu bora zaidi katika mchezo wa kikapu barani Afrika na wana matumaini makubwa ya kutwa medali mwaka huu. Pamoja na timu hiyo, Angola inapeleka London waogeleaji wawili.

Benin inatuma waogeleaji wawili na wanariadha wanariadha wawili kadhalika pamoja na mshindani mmoja wa mchezo wa taekwando.
Nyota inamuwakia Amantle Montsho, mwanariadha wa Botswana ambaye ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 400, ambaye huenda akaipatia nchi yake medali ya kwanza kwenye mashindano hayo.

Msichana huyo mdogo amejijengea stamina kwa kukimbizana na mbuni kwenye makonde makavu wakati akienda shuleni kaskazini mwa Botswana.

Baba yake ni mfanyabiashara anayemiliki duka dogo la bidhaa za rejareja na hakuamini alipopelekewa taarifa, kwamba bintiye anakimbia kwa kasi kama mvulana!
Burkina Faso inawakilishwa na wachezaji sita watakaoshindana kwenye riadha, fencing, kuogelea na judo. Cape Verde itawakilishwa na mwanasarakasi na bondia kwenye Olimpiki. Kama ilivyo kwa nchi nyingine ndogo za Afrika, Cape Verde ina wakati mgumu kugharamia wanamichezo wake.

Misri imefuzu kwa mchezo wa kuogelea wenye manjonjo ya aina yake, kama waogeleaji kucheza dansi au sarakasi majini. Kadhalika itawakilishwa kwenye kulenga shabaha, badminton, ngumi, mpira wa mikono, kupiga makasia na sarakasi.
Ushiriki wa Misri si haba, kwani nchi hii ya Afrika Kaskazini ina zaidi ya wanamichezo 100, na ingawa si wengi wana nafasi ya kutwaa medali, itavutia kuifuatilia timu yenyewe.

Ethiopia, kama ilivyoelezwa awali, ina nafasi kubwa ya kutwaa medali kadhaa za dhahabu. Haile Gebrselassie ni moja ya nyota wake, akikimbia mbio ndefu na ameshapata medali ya dhahabu mara mbili na sasa anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za nyika.
Yupo mwingine – Kenenisa Bekele aliyetwaa medali ya dhahabu mwaka 2008 anayechuana tena kulinda heshima au hata kuvunja rekodi.
Ethiopia itakuwa na wanamichezo 34, baadhi wakipewa nafasi kubwa ya kutwaa medali za dhahabu. Si ajabu wakatwaa dhahabu kwenye mbio za mita 10,000.
Washiriki wake, isipokuwa mmoja wanashindana kwenye mbio ndefu na za kati.
Mmoja ni bondia, Molla Getachew anayepigana katika uzito mwepesi wa unyoya. Huyu hamiliki hata gloves za kupigana, bali huazima kwenye kituo kibovubovu cha mazoezi anakojifua.

Guinea ya Ikweta nayo inashiriki Olimpiki mwaka huu, ikiwa na wachezaji watatu – mmoja wa judo na wawili wa riadha.
Vipi kuhusu Eritrea? Licha ya umasikini wake uliokithiri, mwaka huu inapeleka wachezaji 11 London, wengi wao wakiwa wanariadha. Tumaini lao kubwa lipo kwa mkimbiaji wa mbio ndefu Zersenay Tadese.

Gabon iliyokuwa mwenyeji mwenza wa mashindano ya Kombe la Mabingwa Afrika mwaka huu inapeperushiwa bendera yake na mshindani mwanamama kwenye judo, bondia na wanariadha kadhaa.

Gambia itakuwa na wanariadha wawili na bondia mmoja.
Ghana inawinda medali kwa kupeleka mabondia watano, wanariadha wawili, akiwamo mrukaji aitwaye Ignatius Gaisah anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa medali.

Mabondia wa Ghana wanafanya vyema chini ya kocha wao kutoka Cuba, Roberto Ibanez Chavez, aliyefanikiwa kwa kiasi kikubwa kurejesha hadhi ya mchezo huo Ghana.

Nyota nyingine ya Afrika ni Kenya, kwani imekuwa na mafanikio michezoni katika ngazi za kimataifa, huku kikosi chake kinachotinga London majira haya ya joto kikiwa na watu 80.

Humo kuna wanariadha 36, waogeleaji, mpiga makasia, mabondia na mchezaji wa taekwondo.
Matarajio ya medali kwa Kenya yapo zaidi kwa wanariadha wa mbio ndefu – mbio za nyika zikitarajiwa kuleta matunda, kwani Wilson Kipsang na Mary Keitany walifunika na kuibuka na medali kwenye mashindano ya mbio za nyika yaliyofanyika London mwezi Aprili.

Hakuna wasiwasi kwa wanariadha wengine, kwani wote wamepata maandalizi mazuri. Wengine wanaotakiwa kuchungwa na washindani wao ni pamoja na Robert Cheruiyot (mbio ndefu/mbio za nyika) na msichana mdogo Pamela Jelimo anayekimbia mbio za mita 800 aliyeshinda karibu kila alikoshiriki katika majira haya ya joto.

Mwingine ni Ezekiel Kemboi aliyebobea kwenye kuruka viunzi; Edwin Cheruiyot Soi mbio za mita 5,000; David Rudisha na Wilfred Bungei wanaoshiriki mbio za mita 800 wanaume.

Wapo washiriki wengine wengi wenye fursa nzuri za kushinda kwenye mashindano haya muhimu, na kwa ujumla Kenya ina kikosi kinachotarajiwa kutoa ushindani mkubwa, hivyo kuvutia watazamaji.

Madagascar inapeleka wanariadha kadhaa, mcheza judo, bondia, waogeleaji wawili. Mwogeleaji wa kike, anatarajiwa kuwapa wakati mgumu watangazaji, kwani jina lake ni refu kupita kiasi – anaitwa Aina Andriamanjatoarimanana.

Malawi ina waogeleaji wawili na wanariadha wawili pia. Mwogeleaji mmoja ana umri wa miaka 14, Zarra Pinto anayesoma Shule ya Sekondari ya St. Andrews jijini Blantyre. Nchi hii ya kusini mwa Afrika haitarajii kupata medali, lakini yapo matumaini ya kukua kimichezo kwa siku zijazo.

Mali ina timu nzima ya mpira wa kikapu inayokwenda London pamoja na waogeleaji wachache na mwanariadha mmoja.
Mauritania imefanikiwa kupata wanariadha wawili wakati Mauritius itawakilishwa na washiriki tisa kwenye medani tofauti, ikiwamo badminton na kurusha mikuki.
Morocco imejizatiti, kwani safari hii ina kundi la washiriki 50, wengi wao wakiwa wanariadha. Matumaini yake ya kutwaa medali ni kwa wanariadha wa mbio ndefu na wale wa mbio za nyika.

Amine Laalou anayekimbia mita 800 pia anapewa nafasi kubwa kunyakua medali.
Msumbiji inaingia kwenye michuano hii na waogeleaji wanne, mwanamieleka mmoja, wanariadha wawili, mmoja maarufu katika mbio za mita 800 – Maria Mutola, akishiriki kwa mara ya sita kwenye Olipiki, jambo ambalo si la kawaida.

Sura ya Namibia kwenye Olimpiki hii ni shujaa wake, Frankie Fredericks, na pamoja naye, wapo washiriki wengine waliofuzu katika michezo ya kulenga shabaha, kuendesha baiskeli, ndondi na riadha.

Nigeria imepanga kutafuta mataji kwa kupeleka washiriki katika michezo tofauti, wakiwamo wanariadha wa mbio fupi. Wawili kati yao walishawahi kupata medali, nao ni Olusoji Fasuba na Damola Osayemi.

Nigeria inapeleka pia timu mbili za soka (wanaume na wanawake) na wanatarajia kutoa ushindani mkubwa kwenye masumbwi, mpira wa meza, judo, mieleka, kunyanyua vitu vizito, taekwondo, badminton na kuogelea.

Rwanda ina waogeleaji wawili na wanariadha kwa idadi hiyo hiyo.
Ama kwa upande wa Senegal, ina washiriki 16 wanaokwenda kwenye Olimpiki hii, wakijigawa katika michezo ya kuendesha mitumbwi, judo na taekwondo. Mwanariadha Aminata Diouf ni mmoja wa walio tishio na hii ni michuano yake ya Olimpiki ya tatu kushiriki.

Somalia ingalipo, na inapeleka wanariadha wawili ambao kwa kweli wanatarajia kutwaa medali za dhahabu. Kambi yao ya mazoezi ni imo kwenye kiwanja kikuu kuu kaskazini mwa Mogadishu.

Afrika Kusini si nchi ya kutania kwenye michezo. Wamewekeza hasa, na umakini wake unaonekana katika kikosi chao, ambacho ni kikubwa kuliko nchi nyingi zote barani Afrika.
Wamepanga kupeleka washiriki 225 London, wakiwa wamefuzu kwenye michezo kama wa magongo, kulenga shabaha, kuogelea, riadha, bmx, kupiga makasia, mashindano ya mitumbwi, kufyatua mishale kutoka kwenye pinde, mieleka na kuendesha baiskeli.
Moja ya habari kubwa zaidi za michezo za kuvutia nchini humo ni kuhusu mwanariadha wa mbio za mita 400, Oscar Pistorious. Alikuwa anakaribia kufuzu kushiriki Olimpiki, lakini cha kushangaza ni kwamba hana miguu na watu humwita mkimbiaji bapa.

Miguu yake imekatika, hivyo hutumia ya bandia ijulikanayo kama Cheetah Blades.
Mwaka 2008, mwogeleaji wa masafa marefu, Natalie du Toit alipamba vichwa vya habari baada ya kufuzu kwa Olimpiki, akiwa mwanamke wa kwanza aliyekatwa miguu kufanya hivyo tangu zama za Olivér Halassy mwaka 1936.
Afrika Kusini inao waogeleaji 24 na mpiga mbizi mmoja, wote wakiingia kwa kujiamini kwenye Olimpiki hii.

Ronald Schoeman ni mahiri na anapewa nafasi kubwa ya kutwaa medali, kama ilivyo kwa wenzake, Suzaan van Biljon na Gerhard Zanberg wanaoogelea kwa kurudi nyuma.
Sudan inaingiza washindani saba kwenye Michezo ya Olimpiki, wakiwamo wanariadha kutoka kipande cha nchi hiyo kilichochakazwa kwa vita cha Darfur.

Pamekuwapo na miito ya kuizuia Sudan kushiriki michezo hii, kutokana na hali ya kisiasa ilivyokuwa Darfur wakati wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008.
Hata hivyo, kama mshiriki mmoja alivyosema wakati ule: “Kuna habari nimesikia, lakini ukweli ni kwamba hazinihusu. Sisi sote ni Wasudani, nami nakimbia kwa ajili ya Sudan.”
Mshiriki huyo alisema hayo wakati wa mapumziko, akiwa kwenye mazoezi katika uwanja wa riadha uliokuwa umejengwa nusu nchini mwake.

Mwaka 2008 Sudan ilipata medali moja tu – ya fedha kwa mwanariadha wa mbio za mita 800. Mwaka huu, mwanaridha Abubaker Kaki anatumaini kusigishana na Wakenya kwenye mbio hizo ili aipatie nchi yake medali ya dhahabu.

Hata hivyo, washiriki wa Sudan wanakabiliwa na uhaba wa viwanja vya mazoezi na kwa kiasi kikubwa wanafadhiliwa na vikundi vya hiari vya Uingereza.
Hali hii ni tofauti kabisa na jirani zao wa Ethiopia na Kenya wenye viwanja vizuri na mipango thabiti ya mazoezi kwa wanamichezo wake. Kadhalika kuna fursa nyingi za ufadhili zinazotolewa kwa mshiriki mmoja mmoja.

Togo inayotuma washiriki wawili ni mfano anuai wa nchi ya Afrika isiyokuwa na fedha za kuwadhamini wanamichezo wake kwa ajili ya Olimpiki.
Tunisia ina kikosi kikubwa kwa ajili ya michezo hii, wakiwamo watakaoshiriki riadha, ndondi, mashindano ya mitumbwi, kuogelea, mieleka, mpira wa meza na mingine mingi. Kwa ujumla wana washiriki 32 katika michezo 10.

Uganda ina msafara usio mdogo, kwani itaingiza washiriki 11 katika michezo minne, kama vile waogeleaji, wanariadha na yumo mchezaji namba moja wa badminton Afrika, Edwin Ekiring.

Zambia inaingiza mwanamasumbwi mmoja na wanariadha sita wanaotarajia kujifanya vyema, hata kama hawatazoa medali safari hii. Atakuwapo pia mchezaji mmoja wa badminton.

Licha ya hali tete ya kisiasa nchini Zimbabwe, taifa hilo linapeleka washiriki 13 London, likiwamo tegemeo lake kubwa – Kirsty Coventry.
Huyu alishinda medali tatu kwenye mashindano ya Athens, Ugiriki mwaka 2004 na ndiye anashikilia rekodi ya dunia katika kuogelea kwa kurudi nyuma.

Baada ya mafanikio yake kwenye mchezo huo, watoto kadhaa waliozaliwa nchini mwake walipewa jina lake – Kristy – baadhi wakipewa jina la katikati la Coventry, na hata wengine wakiitwa ‘Goldmedal’ au ‘Threemedals’, ilimradi kusherehekea mafanikio yake aliyopata Ugiriki.

Hiyo ndiyo hali ya Afrika, na hayo ndiyo matarajio ya kufanya vizuri au vibaya; kusuka au kunyoa; kupwa au kujaa kwa Afrika kwenye michuano hii mikubwa duniani.
saria@tanzaniasports.com

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version