Menu
in

Afrika iongezewe nafasi kombe la Dunia

ALHAMISI ya Juni 18,2009,dunia ilitikisika kwa kishindo kizito kilichotokea katika uwanja wa Ellis Park,jijini Johannesburg,Afrika Kusini baada ya mabingwa wa dunia wa soka,Italy kulala kwa bao 1-0 toka kwa Waafrika wa Misri kwenye mashindano ya mabara yanayofanyika nchini Afrika Kusini mwaka huu.

Aliyesababisha mtikisiko huo wa dunia ni mchezaji Mohammed Hommos anayechezea klabu ya Ismailia ya Misri aliyepachika kwa kichwa bao pekee la mchezo huo kwenye dakika ya 39.Hii ni mara ya kwanza kwa mabingwa wa soka wa dunia, Italy kufungwa na timu kutoka Afrika,bara lililo juu kwa sasa kisoka lakini lisilopewa thamani inayostahili!

Hii si mara ya kwanza kwa timu ya Afrika kuwafunga mabingwa wa dunia.Itakumbukwa kwamba mwaka 1990 kwenye fainali za kombe la dunia nchini Ujerumani,Cameroon iliwafunga 1-0 Argentina,mabingwa wa dunia waliokuwa wakitetea kombe lao. Mwaka 1996,Nigeria iliwafunga 2-1 mabingwa wa dunia wa wakati huo,Brazil kwenye mashindano ya Olympic,Atlanta,Georgia,Marekani. Vipigo kwa mabingwa wa dunia toka kwa Waafrika havikuishia hapo kwani mwaka 2002,kule Seoul, Korea,Waafrika kutoka Senegal waliwalaza1-0 Ufaransa,mabingwa wa dunia,waliokuwa wakitetea kombe lao.Safari hii tena Waafrika wengine wamefanya kweli kwa mabingwa wengine wa dunia huko Afrika Kusini.

Si jambo la kubishaniwa kabisa kwamba kwa sasa Afrika iko juu sana kisoka ikithibitishwa na ukweli kwamba wachezaji wa bara hili wamekuwa wakitoa mchango mkubwa mno wa mafanikio ya klabu za Ulaya.Ubora wao ndiyo unaofanya timu zao nyingi za Taifa zisizigwae timu zozote za Taifa toka nje ya bara hili, zikiwemo mabingwa wa dunia.Kinachosikitisha, licha ya ukweli huo kuonekana wazi, dunia haioni haja kwa bara hili kuongezewa idadi ya timu za kushiriki fainali za kombe la dunia. Kwa jinsi soka ya Afrika ilivyo juu kwa sasa, timu tano kwenye fainali za kombe la dunia ni chache mno ukizingatia,pamoja na ubora wa soka ya bara hili kwa sasa,ukubwa wake na wingi wa nchi zake.

Nafasi tano kwa Afrika zinafanya baadhi ya nchi za Afrika zenye uwezo wa kuleta ushindani wa kweli kwenye  fainali ya kombe la dunia kukosa nafasi wakati kuna timu “chovu” toka mabara mengine zinapata nafasi hiyo na kwenda kuitumia hovyo kabisa bila  kuleta upinzani wowote ule na badala yake kuwa chanzo cha uhakika cha pointi na magoli ya kufunga kwa timu stahili za mashindano hayo! Kwa Afrika, Gabon, Togo, Morocco na Cameroon ambazo zina soka ya hali ya juu, ziko kundi moja ambapo mmoja tu ndiye atakwenda kwenye fainali za kombe la dunia,Afrika Kusini, mwakani.Nani aende na kina nani wabaki,wakati wote wanne ni wazuri? Kuna Algeria, Zambia, Rwanda na Misri kwenye kundi moja. Hapo watatu wana uwezo wa kuleta upinzani wa uhakika kwenye fainali za kombe la dunia mwakani lakini nani aende huko kati ya Algeria, Zambia na Misri na kina nani wasiende? Kwenye kundi la Tunisia,Nigeria,Kenya na Msumbiji,nani aiwakilishe Afrika kwenye fainali hizo kati ya Nigeria na Tunisia?

Kinyume chake, kwa Ulaya yenye nafasi nyingi,kuna timu zinapenye kwenda kwenye fainali hizo lakini timu hizo ukizishindanisha na timu za nafasi ya tatu kwenye makundi ya timu za Afrika za kwenda kwenye fainali hizo,nyingi zilizofanikiwa za Ulaya zitapigwa vibaya sana na “walioshindwa” hao wa Afrika! Inakuwaje Afrika iliyo na nchi nyingi ilingane kiidadi ya timu za kucheza fainali ya kombe la dunia na nchi za Amerika Kusini ambazo ni chache kiasi cha Brazil kupakana na nchi zote za bara hilo isipokuwa Chile na Ecuador tu? Mbona nyingi ya timu za bara hilo zinazofanikiwa,ukiondoa mbili tunazoziogopa kwa umaarufu wao za Brazil na Argentina, zina viwango kama vya nchi nyingi za Afrika zisizofanikiwa?

Bara linapokuwa na timu zenye uwezo mkubwa kama Nigeria, Morocco, Algeria, Misri, Cameroon, Ivory Coast, Senegal, Tunisia, Ghana, Afrika Kusini, Angola, Togo,Mali, Gabon, DR Congo na Zambia kulipa nafasi tano tu za kombe la dunia ni kulionea, kulinyanyasa na kulipuuza.Utaratibu huu unazifanya nchi zinazoinuka kisoka barani humu kama Zimbabwe, Sudan,Guinea,Kenya,Msumbiji na Tanzania zisijizatiti kwa mafanikio ya kwenda kwenye fainali za kombe la dunia kwa ukweli usio na chembe ya unafiki kwamba ni kazi ngumu kufikia tano bora ya bara hili.

Lakini nafasi zetu zikivutwa vutwa mpaka 10 au kwa hatua angalau tuanzie nafasi nane,kidogo ndoto ya kufikia hapo inaweza kujakuja kwa kina sisi na hivyo mipango yetu itakuwa ya uhakika zaidi kwani itakuwa ya “kifainali za kombe la dunia”.Ukiwa na mipango ya ukubwa huo,ni wazi utaanza kufanikiwa kwa madogo kama kucheza fainali za mataifa ya Afrika ya wachezaji wote (CAN).

Kwa hiyo,nawaomba waafrika wenzangu wa Tanzania wenye nafasi ya kuhudhuria vikao vya CAF kuipeleka hoja hiyo kwenye vikao hivyo ili ifikishwe FIFA kwa kuzingatia wingi wa nchi za bara hili,idadi kubwa ya nchi zinazoweza kuleta upinzani mkubwa kwenye kombe la dunia inayozidi 10 kwa sasa toka bara hili na umuhimu wa kuongeza idadi ya timu za fainali ya kombe la dunia toka 32 za sasa hadi 40 ili kuongeza hadhi ya mashindano haya makubwa kuliko yote ya soka duniani,yanayohusisha dunia nzima kila baada ya miaka minne.Badala ya timu nne kila kundi kwa makundi manane (A-H),basi ziwepo timu tano kwa kila kundi na shamrashamra hizo za dunia nzima za mara moja kwa miaka minne zichukue muda mrefu kidogo zaidi ya sasa.

Tatizo letu waafrika ni kwamba ili tupate kitu chochote, hata kilicho halali au haki yetu, huwa tunasubiri kufikiriwa na wakubwa.Hii ni tangu baadhi ya nchi za kiafrika zilivyopewa uhuru kwa maamuzi tu ya watawala wao mpaka kuongezewa kidogo kidogo idadi ya timu za kucheza fainali ya kombe la dunia hadi kupewa nafasi ya kuandaa fainali hizo mwakani! Huwa hatuombi sana bali huwa tunasubiri kufikiriwa.

Mafanikio ya kupata kinachohitajika,hutokana na juhudi za anayehitaji na wala si huruma au uelewa wa mwenye nguvu ya kutoa hicho kinachohitajiwa.Tusisubiri dunia ione kuwa Misri ya Afrika iliyotoka kufungwa 3-1 na Algeria ya Afrika iliwafunika vibaya sana Wabrazil wanaoheshimika sana duniani kisoka kwa kufunga magoli matatu ya “move” tupu ya gonga za kutoka nyuma licha ya kulala 4-3.

Kwa nini waafrika tunasubiri wakubwa waone kuwa Wamisri hao wanaweza wasiende kwenye fainali zijazo za kombe la dunia na nafasi hiyo wakaipata wakali wengine,Algeria,walio nao kundi moja? Kwa nini Waafrika tusipiganie hoja ya kuongezwa kwa timu za bara letu kwenye fainali ya kombe la dunia? Ni ukweli usiopingika kwamba nafasi tano kwa Afrika kwenye fainali za kombe la dunia,kwa sasa zimepitwa na wakati kwa mbali sana.

Ibrahim Mkamba [ibramka2002@yahoo.com]

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version