Menu
in , , ,

ADAM JOHNSON NA WAJIBU WA WACHEZAJI MAARUFU KWA JAMII

Tanzania Sports

Wapo wachezaji ambao huwa hatujawasikia kabla ya kufanya vituko nje ya taaluma zao. Mwaka 2012 tulimsikia Frabrice Muamba wa Congo DRC alipoanguka uwanjani wakati wa mechi kati ya timu yake ya Bolton Wanders na Tottenham Spurs. Alipatwa na mstuko wa moyo uliosimama kwa dakika 78. Baadaye ilibidi ajiuzulu kutokana na ushauri wa waganga. Muamba amefahamika sana si kwa mpira wake – aliowahi kuchezea Arsenal na Bimimgham. Kutokana na tukio hilo  tumemfahamu. Baada ya kustaafu alikwenda kusomea uanahabari wa michezo  na kufuzu shahada ya kwanza  BA Honours.

Mwingine aliyefahamika kwa vituko alikuwa Joey Barton.Licha ya kwenda jela kwa kumpiga mwananchi mmoja ngumi ishirini hadi akazimia usiku akiwa na binamu zake, Barton alifungwa miezi sita mwaka 2008. Aliwahi kupigana na dereva wa teksi, akampiga ngumi mchezaji mwenzake Ousmane Dabo – wakati akichezea timu ya Manchester City na vituko vingine vingi. Siku hizi Joey Barton anaichezea timu ndogo ya Burnley. Ingawa ni mchezaji mzuri, makocha  taifa la England wamekuwa na wasiwasi kumweka kundini asije leta fyoko.

Tukija kwenye mambo ya ngono mshambuliaji Ched Evans bado angali jela kutokana na madai alimbaka msichana wa miaka 19 akiwa amelewa. Ched Evans aliyekuwa Sheffield United – ambayo haijulikani kama  Man United, Arsenal na Chelsea, alizua mtafaruku wakati kesi yake ikiendelea mwaka juzi. Gazeti hili lilimwandika sana alipojitetea kuwa dada huyo alitaka mwenyewe ngono kisha akapiga kelele kaliwa mkuku. Vilio vya akina mama vilisikika na kusambaza jina la Ched Evans na kabla ya kufungwa klabu zilizoelekea kutaka kumsajili  zilitishiwa na wananchi waliodai hatuwezi kuwa  na watu maarufu wanaodhalilisha madem.

Hayo ndiyo yaliyomtokea Adam Johnson aliyekuwa bawa (winger) wa timu za Manchester City (2010) na Sunderland. Johnson anakabiliwa na shtaka la kufanya mapenzi na dogo wa miaka 15. Kabla hatukuwahi kumsikia Adam Johnson. Hata wanaoshabikia sana wachezaji walimjua lakini si kiasi cha kuliimba jina lake. Ila kwa wilaya aliyokulia na kuchezea pale Sunderland- Adam Johnson alikuwa nyota mashuhuri na si ajabu mtoto huyo aliye bado shule, akamshabikia.

Kelele zinapigwa afungwe, afungwe. Tayari mkataba wake umeshafutwa, mshahara wake wa paundi 60,000 kwa juma umezimwa, na wiki hii magazeti ya hapa Uingereza yamezungumzia mshahara wa jela ambapo mfungwa hupewa paundi 4 kwa juma …senti za madafu  ukilinganisha na  manoti aliyozoea kusomba Manchester City na Sunderland. Kisa kilianza kutokana na msichana huyo alipoanza kumfuata fuata jamaa na hatimaye wakaanza kutumiana SMS katika simu. Adam Johnson ambaye ana bibi tayari na mtoto mdogo, hakujivunga akafanya vitu na kigoli tena ndani ya gari yake.
Leo magazeti yanazungumzia maisha ya Adam Johnson jela kubwa ya Frankland. Jela  inao wafungwa wakatili maarufu ambao wengi wameua watoto au kubaka wasichana wadogo. Kati yao ni Ian Huntley na Levi Bellfield  wanaoendelea na kifungo cha maisha.

Jela la Frankland linasifika pia kwa wafungwa kupigwa hadi kuuawa na wenzao shauri kwa majambazi hakuna kitu cha chini kama kubaka au kulawiti watoto wadogo.

Hapa utaona namna maisha ya mtu maarufu siku hizi ni jambo la mfano wa jamii na namna tabia zao nje ya taaluma zinavyoweza kufunika vipaji vyao, asilia.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version