UKUBALI au ukatae, lakini mnyonge mnyongeni ila haki zake mpeni. Hapa tulipo hatuwezi kushangilia mambo mabaya tu kwenye mpira wa miguu hasa upande wa waamuzi. Katika mpira wa Tanzania yapo masuala mengi ya kujifunzia kwa mwaka 2024 katika mpira wa miguu kwa sababu nchi hii imeshuhudia wimbi la soka safi, viwango vya wachezaji na furaha tele kutoka kwa mashabiki huku wakiwa na kila sababu ya kusubiri au kuota siku moja makombe ya Timu za Taifa yatakuwa hapa nchini. Huenda wengine wakaona ni ndoto za mchana lakini bila kuziota hizo ndoto hakuna dhamira au shauku ya kuzikamilisha.
TANZANIASPORTS imefanya tahmini katika soka la Tanzania na kubaini kuwa yapo masuala mengi ya kusisimua kwenye mashindano mbalimbali. Kuanzia ngazi za vilabu hadi Timu za Taifa Ligi Kuu Tanzania imetuma ujumbe mzito ambao majirani kama vile Kenya, Uganda, Rwanda na Zambia wameanza kupatwa na kiwewe. Baadhi ya mashabiki wa soka nchi hizo kwenye mitandao mbalimbali wana kiri kuwa soka la Tanzania linazidi kupiga kwa mamboyalitotokea mwaka 2024. Katika makala haya TANZANIASPORTS inakuletea masuala muhimu yanayolitanagza soka la Tanzania kote duniani katika mashindano 7 ambayo wamefuzu na kuwaacha hoi maelfu ya mashabiki wa kandanda barani Afrika.
AFCON 2025
Taifa Stars iliwapa furaha mashabiki wa soka baada ya kuichapa timu ngumu na yenye nyota wanaocheza soka la kulipwa barani ulaya, Guinea kwa bao 1-0 lililofungwa na Simon Msuva. Kwa ushindi huo Tanzania ilijiandikia rekodi ya tatu kufuzu mashindano hayo mfululizo kuanzia mwaka 2019, 2023 na 2025. Bila kujali aina ya wachezaji waliotumikia kikosi hicho lakini ukweli ni kwamba mashindano ya AFCON ni jukwaa muhimu la kuonesha vipaji na kuitangaza nchi kupitia mchezo wa soka zaidi ya filamu ya The Royal Tour. Timu inaposhiriki mara kwa mara inawavutia wataalamu na wachezaji mbalimbali kutaka kujua fursa zinazopatikana kwenye Ligi yetu. Kwa hiyo kufuzu AFCON ni ujumbe mwingine kuwa Tanzania ina vipaji vya soka na ambavyo vinaweza kuwa kivutio kama zilivyo mbuga zetu.
ASFC U-15
Kana kwamba haitoshi, vijana wadogo wa shule walifanya jitihada za kufuata nyayo za kaka zao wa Taifa Stars kwenye kandanda. Tanzania imefuzu mashindano ya Afrika kwa shule za sekondari chini ya miaka 15. Mashindano hayo ni maarufu kama African Schools Program (ASFC). Si kwenye timu za wakubwa pekee bali hata kwenye kikosi cha vijana kama hawa wametuma ujumbe mzito kote duniani na ambapo unawajulisha kuwa si suala la mbuga za Serengeti, Ruaha, Selous, Ngorongoro pekee bali kwenye kandanda wanaweza kufanya kitu muhimu sana. vijana hawa wamefuzu na kudhihiri kuwa mwaka 2024 ulikuwa na shangwe nyingi sana kwenye kandanda Tanzania na zaidi hata majirani zetu wanaona wivu juu ya mafanikio yao.
AFCON 2025 SERENGETI BOYS
Kutoka vijana wa shule za sekondati tunaingia kwenye kikosi cha timu ya Taifa chini ya miaka 17. Timu hii imekuwa na uzoefu wa kushiriki mashindano hayo mara kwa mara lakini mwaka 2024 waliandikwa rekodi nyingi ya kuungana na kaka zao wa Taifa Stars kwa kufuzu mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2025). Wakati mataifa jirani na Afrika wakiwa wanajiuliza kulikoni nchi yetu inafuzu namna hii? Jibu wanalokuja nalo kuwa Ligi Kuu Tanzania inapiga hatua kubwa sana.
“Mpira wa Tanzania unakua kwa kasi sana. Tanzania imefuzu mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana mara mbili, kuanzia yale ya mashule na haya ya chini ya miaka 17. Si ajabu wakichukua kombe la AFCON siku moja,” alisema mmoja mwanahabari kutoka Afrika kusini.
AFCON NGORONGORO HEROES U-20
Kwa mara nyingine tena soka la Tanzania kuanzia ngazi ya chini limeonesha mwelekeo mzuri baada ya kikosi cha timu ya Taifa chini ya miaka 20 maarufu kama Ngorongoro Heroes yaani mashujaa wa Ngorongoro kimefanikiwa kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Mashindano hayo yatashuhudia vipaji vya soka la Tanzania kama ilivyokuwa kwa wakubwa zao wa Taifa Stars.
BSAFCON
Wakati wengi wanashangaa jinsi timu za Taifa za soka zinafuzu maajabu mengine yakaongezeka baada ya kushuhudia soka la ufukweni nalo likituma ujumbe namna Tanzania ilivyojaliwa vipaji. Timu ya Taifa ya soka la Ufukweni nayo imefuzu kwa mashindano ya AFCON. Hii ina maana kuanzia soka la ufukweni hadi viwanjani Tanzania inatamba na inaweza kuwika zaidi kadiri miaka inavyokwenda. Hili lilikuwa jambo la kujivunia kwa mwaka 2024.
CHAN
Tangu enzi za Marcio Maximo, yule mwalimu mahiri wa kandanda kutoka Brazil alipoipeleka timu yetu kwenye mahsindano hayo, kwa mara nyingine tena Taifa Stars imefuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN). Angalau mashindano hayo pia Taifa Stars ina rekodi nayo mara kadhaa lakini mwaka 2024 waliongeza rekodi ya aina yake kwa kufuzu pamoja na mashindano mengine ya Afrika. Hii ina maana Taifa Stars itakuwa ‘busy’ sana kwenye mashindano mbalimbali Afrika.
WAFCON
Hakuna ubishi kwamba timu ya Taifa ya wanawake wa Tanzania inacheza kandanda safi sana. umahiri wao umeoneshwa kwenye mashindano mbalimbali waliyobahatika kushiriki yakiwemo COSAFA. Lakini mwaka 2024 Timu ya Taifa ya wanawake nchini maarufu kama Twiga Stars nayo iliungana na kaka zao kwa kufuzu mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa upande wa wanawake (WAFCON).
Huu ni ujumbe tosha kwa timu za Afrika kwamba Tanzania na mpira wake inakuja kuwashika sio tu kwenye mashindano ya ngazi ya klabu bali hata timu za Taifa. Kwa mwenendo huo vipaji vinahitaji ulinzi tu mengine yanawezekana.