*Yanga wamemrejesha Chuji, Kiiza naye fiti
*Barcelona wapigwa nyumbani Nou Camp
Wekundu wa Msimbazi, Simba wamesafisha mwezi kwa kuwakandika maafande wa Oljoro JKT mabao 4-0 huku wakiwasikilizia wapinzani wao Yanga leo.
Mabao ya Simba kwenye mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Taifa yalifungwa na Amisi Tambwe aliyepiga na hat-trick na kuondoka na mpira, akisema hakutarajia kufunga mengi hivyo.
Bao jingine la Simba lilifungwa na Jonas Mkude na jitihada za Oljoro kutumia mbinu za kiraia na kijeshi chini ya kocha Hemed Morocco hazikufanikiwa hata kidogo.
YANGA NA MBEYA, CHUJI, KIIZA WARUDI
Wakati Simba wakishinda Jumamosi hii, vijana wa makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Yanga Jumapili hii wana kipute dhidi ya Mbeya City.
Hadi watakapoingia uwanjani Jumapili hii, Mbeya City wanajivunia kwa kutofungwa mechi yoyote tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya Tanzania.
Kocha Juma Mwambusi anasema anawajua Yanga ni timu kubwa, anawaheshimu pia kwa sababu ni mabingwa watetezi lakini kwamba hata wao Mbeya wana heshima na anaamini mchezo utakuwa mgumu.
Yanga walikwenda Bagamoyo kujiandaa kwa mechi hiyo baada ya kutoka suluhu mjini Tanga walikocheza na Coastal Union.
Kadhalika waliamua kumrejesha kundini kiungo mahiri Athumani Idd Chuji huku mshambuliaji matata Mganda, Hamisi Kiiza naye akiwa pia amerejea. Itakuwa juu ya benchi la ufundi kuona kama wacheze au la.
BARCELONA WACHAPWA NYUMBANI
Mabingwa wa Hispania, Barcelona wamepoteza mechi katika uwanja wao wa nyumbani wa Nou Camp kwa mara ya kwanza tangu Aprili 2012.
Jumamosi hii ilikuwa chungu jijini hapo, pale Valencia walipomaliza ubishi wao, huku nyota wa Barca, Lionel Messi na wengine wakiwa ndani. Valencia walikatisha ushindi wa mechi 25 mfululizo katika dimba hilo kubwa na la aina yake.
Valencia pia wanakuwa timu ya kwanza kufunga mabao matatu katika mechi ya ushindani hapo Nou Camp dhidi ya kikosi cha Gerardo Martino. Mabao ya Barca yalifungwa na Alexis Sanchez wakati Messi alifunga kwa penati.
Valencia walipata mabao yao kupitia kwa Parejo, Piatti na Alcácer García .
Barca walimaliza wakiwa 10 baada ya Jordi Alba kuzawadiwa kadi nyekundu kwa rafu mbaya dhidi ya Sofiane Feghouli dakika 13 kabla ya mchezo kumalizika.
Mara ya mwisho Barca kufungwa Camp Nou ni Aprili 2012 walipopoteza mechi kwa wapinzani wao wakubwa nchini humo, Real Madrid kwa mabao 2-1.