WANAOUFAHAMU ukweli huu watakubaliana nasi kwamba Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) ulisaidia sana kuinua michezo nchini hasa utaratibu huo ulipokuwa mwendelezo wa utaratibu ulioanzia shule za msingi wa UMISHUMTA mwanzoni na baadaye UMITASHUMTA.
Ni wazi baada ya mpango huo kudorora, uinuaji wa vipaji vya michezo nchini umedorora na mafanikio ya michezo nchini yamedorora. Kurudisha hali ya mafanikio ya zamani, tunahitaji kuasisi na kuimarisha UMISHUMTA na UMISSETA. Aidha, ipo haja sasa ya kuanzisha Umoja wa Michezo wa Vyuo Tanzania (UMIVYUTA).
Enzi za UMISHUMTA na UMISSETA, kulikuwa na wachezaji wa shule za msingi waliokuwa wakichezea timu kubwa za wakubwa nao kutoa mchango mkubwa wa mafanikio ya timu hizo. Yaani wanafunzi wa shule za msingi za miaka hiyo walikuwa wakubwa na wenye nguvu vya kutosha.
Ukija kwenye Sekondari, baadhi ya vijana wa shule hizo waliweza kuchezea klabu kubwa za nchi, timu za mikoa yao na hata timu ya taifa. Kwa mfano timu ya Taifa ya vijana iliyobeba mwezi Mei 1974 kombe la Vijana nchini Uganda ilikuwa kama timu ya UMISSETA ya mwaka huo kwani wachezaji wake wengi kama Zaharan, Lucas Nkondola, Jella Mtagwa, Godfrey Nguluko, Mwinda Ramadhan na wengine walikuwa bado wanafunzi. Wengi wa wachezaji hao walihamia na kocha wao Marijan Shaaban Marijan kwenye timu ya Taifa ya Tanzania Bara na kubeba kombe la Chalenji jijini Dar es Salaam mwezi Oktoba mwaka huo 1974.
Nakumbuka wakiwa Shycom, Shinyanga, Nkondola na Abdallah Mwinyimkuu walikuwa wanaenda kuchezea Simba wakati wa likizo. Mshambuliaji hatari wa miaka hiyo Ali Katolila, alijulikana mpaka kusajiliwa Pan African akiwa mchezaji wa timu ya mkoa wake wa Kigoma kwenye mashindano ya Taifa Cup mwaka 1976 yaliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana Mwanza. Wakati huo Katolila alikuwa bado mwanafunzi.
Kiungo wa kutegemewa wa wakati huo wa Coastal Union, Salim Omar, alifikia mpaka kuchaguliwa kwenye timu ya taifa akiwa mwanafunzi wa sekondari mjini Tanga! Marehemu Gibson Sembuli, akiubeba mkoa wake wa Morogoro kwenye kombe la Taifa mwaka 1970, alikuwa anasoma sekondari mjini Morogoro.Morogoro ilibeba kombe hilo mwaka huo, Sembuli akiwa mfungaji bora wa mashindano.
Enzi zile, timu za Sekondari zilikuwa zinapambana na timu za wakubwa kwenye mashindano makubwa. Kwa mfano, Sekondari ya Kwiro, Mahenge ilikuwa mara nyingi mabingwa wa soka wa Wilaya ya Ulanga, Mkoani Morogoro. Timu hiyo ilishiriki mashindano ya kutafuta ubingwa wa mkoa na matimu kama Mseto, Nyota Afrika, Shujaa, Yetu Afrika na nyingine yenyewe ikiwa tayari na wachezaji wakubwa kama Zuberi Magowa na Hamis Kamungu.
Timu ya shule ya Sekondari ya Tambaza nayo. Hii ilikuwa moja ya timu chache za kuzibabaisha Yanga na Simba miaka hiyo. Nyingine chache zilikuwa Mwadui ya Shinyanga kwa Yanga, Coastal Union, African Sports za Tanga na Cosmopolitan ya Dar es Salaam.
Tukumbushane pia kwamba mwanariadha kijana Gidemis Shahanga alituletea medali toka mashindano ya Jumuiya ya Madola, Montreal Canada mwaka 1978 akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili kwenye shule ya Sekondari ya Mazengo, Dodoma!
Leo hii, kwa maendeleo makubwa tuliyofikia, mtoto wa miaka 12 yuko darasa la saba. Miaka 16 kidato cha nne. Miaka 18 anamaliza kidato cha sita. Huu wa miaka 18 ni umri ambao zamani wanafunzi wengi ndiyo walikuwa darasa la saba, kama si la sita au la tano! Kwa hiyo timu ya UMISSETA kwa miaka hiyo ilikuwa na wachezaji wengi wa umri wa miaka 20 mpaka 23. Leo hii, kwa UMISSETA, utakuwa na wachezaji wengi wa umri wa miaka 13-16 umri wa vitoto vya UMISHUMTA enzi zile!
Kwa msingi huo, tunaona kama tuna nia ya dhati ya kuweka msingi wa michezo toka kwenye taasisi za elimu, uanzishwe utaratibu wa kuwa na Umoja wa Michezo wa Vyuo vya elimu ya juu nchini (UMIVYUTA) kwani umri wa vijana wetu wengi vyuoni humo kwa sasa ndiyo ule wa vijana wa Sekondari miaka ile. Umri huu ndiyo hasa wa kucheza mashindano ya ushindani wa kweli.
Kwa sasa idadi ya vyuo vya elimu ya juu inalingana na idadi ya sekondari kwenye miaka ya 1970. Aidha, kwa sasa ni kwenye ngazi ya vyuo ndiko utapata mchanganyiko wa uhakika wa vijana toka kona zote za nchi kama ilivyokuwa kwa sekondari za miaka ile. Huu mchanganyiko husaidia kubadilishana uzoefu wa kutoka sehemu tofauti wa nyanja nyingi za kimaisha ikiwemo michezo.
Hili likiwekwa kwenye utekelezaji litakuwa na faida kubwa kwa taifa kuliko hasara. Watu watahoji ugumu wa masomo kwa kiwango hicho cha elimu na ushiriki wa michezo. Si kweli kwamba sasa hivi vijana hao hawafanyi mambo mengine zaidi ya masomo. Wanafanya sana, pamoja na hiyo hiyo michezo lakini kwa michezo si kwa utaratibu maalum. Aidha, wanafanya mambo mengine yasiyo ya msingi kama kujirusha viwanja usiku na vitu vingine vya kuwabomoa ambavyo hawatavifanya wakishiriki michezo kirasmi
Mhandisi Dennis Mdoe akichezea Nyota Nyekundu na Mhasibu Lawrence Mwalusako akichezea Yanga mwaka 1987 walikuwa Chuo Kikuu. Baadaye Mdoe aliungana na rafiki yake Yanga. Wawili hawa walicheza soka ya juu na walifaulu masomo kwa hali ya juu. Mdoe sasa ni Mhandisi tajiri nchini Botswana na Mwalusako ni katibu Mkuu wa Yanga. Kinyume chake wanaoshiriki michezo, huwa na uwezo zaidi wa kimasomo kwani mazoezi ya michezo husisimua mwili na akili.
Naomba wazo hili litupiwe macho kwa mtazamo wa maendeleo ya michezo yote hata kama mifano iliyotumika hapa zaidi ni ya mchezo wa soka.