WACHEZAJI 20 wa Tanzania tayari wamekwishaaga mashindano ya Jumuiya ya Madola yanayofikia tamati Alhamisi mjini New Delhi, India baada ya kupoteza katika michezo yao yote.
Leo ni siku ya tisa tangu kufunguliwa kwa mashindano hayo ambapo Tanzania iliwakilishwa na wachezaji 28, lakini wachezaji waliobaki ambao wanaweza kutufuta machozi ni nane tu ambao kati yao hakuna aliyecheza hata mmoja hivyo bado hawajaonja tamu na chungu ya mashindano hayo. Akizungumza na Mwanachi kwa njia ya simu kutoka New Delhi, Mkuu wa msafara wa Tanzania, Juliana Yasoda alisema kuwa tayari mabondia nane wa Tanzania na waogeleaji wanne wamekwishatolewa. “Wachezaji sita wa Mpira wa Meza wanamalizia tu mechi zao, lakini tayari wamekwishatolewa pia Paraolimpiki mmoja ametolewa na mmoja atacheza leo, lakini tegemeo limebaki kwenye Riadha na mchezaji huyo wa Paraolimpiki. “Wachezaji wetu walijitahidi, lakini bahati haikuwa yao hivyo nguvu zetu zote tumezielekeza kwa wachezaji wetu ambao bado hawajacheza ili angalau waweze kufanya vizuri na kurejea na medali hizo chache za wachezaji waliosalia,” alisema Yasoda. Tegemeo la Tanzania limebaki kwa wanariadha Marco Joseph katika mbio za mita 10,000 na 5,000, Frank Martin anayekimbia mita 800 na Barae Hera anayekimbia Mita 1,500 na 800. Wanariadha wengine ni Shamba Kitin, Samson Ramadhan na Patrick Nyangero watakao kimbia mbio za Marathon (km 42) upande wa wanaume na kwa Wanawake Restituta Joseph atakimbia Marathon (KM 42), pamoja na mchezaji mmoja wa michezo ya walemavu, ambao bado hawajacheza tangu kuanza kwa mashindano hayo. Katika mashindano hayo yaliyofunguliwa rasmi Oktoba 3, Tanzania ilitupa karata yake ya kwanza katika mchezo wa kuogelea Oktoba 4 kwa muogeleaji wake Mariam Foum kuanza vibaya hivyo kufungua dimba bila matumaini huku wachezaji sita wa Mpira wa Meza wakishindwa kutamba siku hiyo hiyo mbele ya Ghana na kuishia kutolewa pia katika hatua za awali. Oktoba 5 wachezaji watatu wa Tanzania pia waliendelea kuwapa simanzi mashabiki wao hapa nchini pamoja na kupoteza matumaini ya kuibuka na Medali nyingi katika mashindano hayo kwa kufanya vibaya. Wachezaji hao ni Sunday Elias na Hashim Saimon (Ngumi), Khalid Rushaka (Kuogelea). Nasser Mafuru na Seleman Kidunda (Ngumi) wiki iliyopita walianza kurejesha matumaini ya Watanzania yaliyokuwa yamepotea baada ya kuibuka na ushindi katika mapambano yao ya awali, lakini walishindwa kung’ara katika hatua ya mtoano juzi na kujikuta wakiaga mashindano hayo. Mbali na wachezaji hao pia mwanariadha Damian Chopa, mchezaji wa michezo ya walemavu Ignas Mtemve, muogeleaji Magdalena Mosha, mabondia Haruna Swaga, Leonard Machichi na Revocatus Shomari wameaga mashindano hayo. |
Comments
Loading…