*Waziri mkuu, Mhe Kassim Majaliwa atoa majibu*
Jumamosi iliyopita nilihudhuria mkutano uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekutana na Watanzania kwenye ukumbi wa Ubalozi wetu hapa London.
Wakati wa maswali nilimuuliza Waziri Mkuu mambo matatu muhimu ambayo bila shaka wapenzi wengi wa michezo na wazalendo kiujumla wangependa kufuatilia.
Mosi ni suala la viwanja kuwa vibovu sana siku hizi. Viwanja hivi vimemilikiwa na mamlaka za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ukweli ni kwamba havifai kabisa. Je, kuna hatua gani kuviboresha?
Swali la pili lilihusu matayarisho ya michuano ya kimataifa.
Muda mrefu nimepata usongo namna ambavyo wachezaji wetu wa kitengo cha kuogelea hufanya vibaya mashindano ya kimataifa. Hisia iliyopo ni kwamba waogeleaji wanakwenda tu ‘kushiriki’ lakini si kuwania medali za ushindi.
Moja ya sababu ni kujitayarisha kimazoezi katika vijibwawa vyenye mita 25 badala ya mita 50 kama inavyokuwa kimataifa. Sasa wakati wa mshikemshike unapowadia hawamudu. Inabakia basi kuwalaumu kwamba wamefanya vibaya.
Swali la mwisho lilihusu vipaji na uwezo, kimajimbo. Makao makuu ya mashindano na sehemu zinapopatikana huduma mbalimbali za wanamichezo ni Dar es Salaam. Lakini jiografia hii haizingatii kwamba kila wilaya, mkoa, eneo au jimbo huwa na watu wenye uwezo au kipaji cha mchezo ya aina fulani.
Pendekezo langu ni kwa watayarishaji wa wanamichezo mikoani wazingatie ujuzi na vipaji vya wenyeji.
Mathalan, ikiwa wachezaji wazuri wa mpira wako zaidi Tanga, Morogoro na Dar es Salaam, hapo basi majimbo haya yangeweka nyundo zaidi kuwanoa wanasoka.
Ukija riadha ni Singida, Dodoma na Arusha ndiyo hodari; hivyo basi, matayarisho ya fani hizi yawe huko huko. Kwa mpira wa kikapu na nyavu, wenzetu wa majimbo ya Mwanza, Biharamulo, Kilimanjaro na Ukanda wa Ziwa humudu zaidi.
Katika kunijibu, Waziri Mkuu Majaliwa alikubaliana kabisa na kauli yangu. Tunabahatika kuwa Waziri Mkuu ambaye kitaaluma mbali na siasa na utawala ni mwanamichezo.
Kuhusu viwanja aliafiki havipo katika hali nzuri chini ya halmashauri na manispaa mbalimbali nchini. “Vingi vina mashimo na vidimbwi vidimbwi…” alisema.
Waziri mhusika, Nape Nnauye ameshalipa suala hilo kipaumbele. Hivi karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesimamia uwekaji wa nyasi katika baadhi ya viwanja kama Nyamagana na Samora.
Jambo la pili ni kuwekezea katika viwanja. Watu binafsi wamesharuhusiwa kuvijenga na kuvishughulikia.
“Lengo ni kuanza na viwanja vichache halafu ndiyo tusonge mbele,” anasema na kuongeza kwamba Zanzibar na Pemba tayari mambo yanatia moyo.
Kuhusu utayarishaji wa michezo kufuatana na uasilia, alikubali pia hoja. Kwa mfano Mbeya kuna vipaji na uwezo wa mbio fupi za ‘sprint’ na kutupa vitufe. Ukija riadha, kama nilivyoulizia kweli Singida, Dodoma, Mbulu na Arusha wako wakimbiaji wazuri hususan wa mbio ndefu.
Waziri Mkuu alitania kuhusu Uchagani (ninakotoka) kule mchezo husika ni mpira wa wavu (Volleyball).
Tukija swali la mwisho kuhusu mabwawa ya kuogelea. Waziri Mkuu Majaliwa alikubali kwamba serikali haijaangalia ipasavyo.
Kwa sasa mabwawa yanayotumika kuwatayarisha waogeleaji wetu yote yako Dar es Salaam: International School of Tanganyika (IST), Kunduchi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ila yote yana urefu pungufu; ni mita 25 kwa mita 25.
Akitania na kukubali; “kila mchezo wa kimataifa tunakuwa wa mwisho.”
Sasa basi tusubiri kwa hamu kauli hii na kuomba Mungu Serikali ya Awamu ya Tano ituondolee adha kwenye michezo yetu.