Arsenal wa pili
Baada ya Leicester kujihakikishia ubingwa mapema, kitendawili cha
nafasi zinazofuata kimeteguliwa kwa Arsenal kuchukua ya pili,
Tottenham Hotspur ya tatu na Manchester City ya nne.
Hii ni mara ya kwanza kwa Arsenal kumaliza katika nafasi hiyo tangu
2005, na wamefanya hivyo kwa namna ya pekee kwa kuwachabanga Aston
Villa 4-0.
Mshambuliaji Mfaransa, Olivier Giroud alifunga mabao matatu na kutaka
kuonesha kwamba bado yumo, hivyo ategemewe msimu ujao na kocha wake,
Arsene Wenger.
Nahodha wa Arsenal aliyekuwa majeruhi na anayetarajiwa kuondoka
kiangazi hiki, Mikel Arteta ndiye alisaidia bao jingine, kwa mpira
wake kumparaza Mark Bunn.
Kwa mtaji huo, Arsenal wamewashusha Spurs waliokuwa wakishikilia
nafasi ya pili kwa kitambo sasa na walikuwa pia wakipigana kikumbo na
Leicester kutwaa ubingwa kabla ya kupatwa majanga ya kufungwa.
“Imetokea tena,” waliimba washabiki wa Arsenal wakifurahia kumaliza
juu ya mahasimu wao wa London Kaskazini – Spurs kwa msimu wa 21
mfululizo. Arsenal wamefuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
(UCL) kwa msimu wa 19 mfululizo, ambako kwa Arsene Wenger ni moja ya
malengo yake.
Katika matokeo mengine siku hiyo ya mwisho ya msimu wa ligi kuu,
Chelsea walikwenda sare ya 1-1 na Leicester, Everton waliomfukuza
kocha Roberto Martinez wakawachakaza Norwich 3-0 na Newcastle
walioshuka daraja wakawatandika Spurs 5-1.
Southampton walitumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kushinda 4-1 dhidi
ya Crystal Palace, Stoke wakawazidi nguvu West Ham kwa 2-1 na Swansea
wakatoshana nguvu na Manchester City.
Watford walienda sare ya 2-2 na Sunderland, West Bromwich Albion
wakafungana 1-1 na Liverpool, wakati Manchester United wanaoshika
nafasi ya sita nyuma ya Southampron watamalizana na Bournemouth
Jumanne hii.
West Ham wamemalizia nafasi ya saba wakat Liverpool ni wa nane, Stoke
wa tisa na Chelsea wa 10, wakiweka rekodi mbaya kwani walikuwa
mabingwa watetezi.
Norwich, Newcastle na Aston Villa wameshuka daraja.