*Jose Mourinho alimwa faini
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter ametangaza kwamba atatetea nafasi yake kwenye uchaguzi ujao mwakani.
Blatter alikuwa akidhaniwa kwamba angestaafu na tayari wanamichezo wengine walianza kufikiriwa kuchukua nafasi yake, lakini amekata mzizi wa fitna akisema anagombea kwa mara ya tano.
Mwaka 2011 alipita bila kupingwa kwenye uchaguzi lakini kwenye uchaguzi ujao inadhaniwa kwamba Blatter (77) atakumbana na upinzani kwenye nafasi aliyoshikilia tangu 1998. Binafsi alipata kusema kwamba anafikiria kutogombea ila sasa amebadili mawazo.
Aliliambia gazeti la nchini mwake Uswisi la ‘Blick’ hivi: “Mimi ni mgombea wa nafasi hii tena. Muda wangu unamalizika lakini kazi yangu niliyotaka kufanya bado.”
Uchaguzi huo utafanyika katika makao makuu ya shirikisho hilo, Zurich nchini Uswisi Juni mwakani.
Makamu wa Rais wa Fifa, Jeffrey Webb na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Jerome Champagne wamekuwa wakitajwa kama mbadala wa Blatter lakini wote wamesema kwamba hawatasimama kushindana na rais wa sasa. Kiongozi wa Uefa, Michel Platini anadaiwa kutaka kumng’oa Blatter hapo Fifa, ili aingize mipango mipya.
MOURINHO APIGWA FAINI £10,000
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amejikuta pabaya baada ya kupigwa faini ya £10,000 kutokana na kauli yake aliyotoa baada ya mechi dhidi ya Sunderland Aprili 19 mwaka huu.
Baada ya kufungwa kwenye mechi hiyo, Mourinho alionekana kumbeza mwamuzi Mike Dean lakini akadai ‘kumpongeza’ kwa kazi nzuri baada ya timu yake kulala kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Chama cha Soka (FA) kimesema kwamba kauli aliyotoa imeiweka soka katika hali tete na kwamba Mreno huyo alionesha tabia mbaya hivyo ni sahihi kuadhibiwa. Mourinho amepoteza rufaa yake aliyokata kupinga kupigwa faini ya £8,000 kutokana na kosa jingine.
Aliadhibiwa baada ya kumwendea mwamuzi Chris Foy wakati wa mechi waliyofungwa na Aston Villa 1-0 na alifanya kitendo hicho baada ya kuashiriwa aondoke kwenye benchi la ufundi na kwenda jukwaani. Tume ya Uratibu wa Soka iliyosikiliza rufaa hiyo imekubaliana na uamuzi wa FA kwamba Mourinho alikosa nidhamu.
Kufungwa kwa Chelsea na Sunderland kulitibua mwenendo wa Chelsea katika kuwania ubingwa wa England, na katika mechi hiyo, kocha msaidizi Rui Faria alitolewa nje na kisha kupigwa marufuku kukaa kwenye benchi la ufundi kwa mechi sita kutokana na kufanya fujo.
Comments
Loading…